Maendeleo na wasiwasi mjini Kabul
9 Agosti 2011Wataliban walipopinduliwa nchini Afghanistan mnamo mwaka 2001, mji mkuu wa nchi hiyo, Kabul, ulikuwa na kiasi ya watu 600,000 tu. Sasa inatathminiwa kuwa takribani watu milioni 4 hadi 5 wanaishi katika mji huo. Hii inatajwa kuwa ni dalili ya kuendelea kwa Kabul. Moja ya sehemu zinazoshuhudia maendeleo haya ya Kabul ni mtaa wa Karte Seh, magharibi ya mji mkuu huo, eneo ambako mashirika mengi ya misaada yana ofisi zake, mtu huweza kuona maendeleo ya hivi sasa.
Hayo ni maendeleo yanayoambatanishwa na utawala mpya na yanayoungwa mkono na wananchi. Kazi za ujenzi zinaendelea katika kila pembe ya Karte Seh. Kwa wengine, makelele ya ujenzi ni usumbufu, lakini kwa Kabul ujenzi ni furaha. Kwani kunapojengwa, vile vile huwekezwa.
Zamani, wakaazi wa eneo hilo walikuwa watu wa tabaka la kati na nyumba za kifahari ni sehemu ya mandhari inayopamba mtaa wa Karte Seh. Baadaye zikaja nyumba za kawaida za udongo - hayo ni matokeo ya vita na watu wa mashambani kukimbilia mji mkuu Kabul. Na sasa, nyumba mpya zinajengwa kwa kuigiza ujenzi wa kifahari wa Pakistan kama vile kuwa na milingoti na kuta za rangi ya fedha na dhahabu. Masikini na matajiri wa Karte Seh hukutana karibu na Pol-e-sorkh yaani "daraja jekundu". Ni mchanganyiko wa kikabila unaovutia. Huko, ni nadra kuona wanawake waliovaa mabaibui yanayofunika mwili mzima. Barabara nyingi kama hapo zamani bado hazina lami, kwa hivyo malori yanayopita barabarani huwatimulia vumbi wapita njia.
Tafauti ya sasa na enzi za Taliban
Sokoni kila muuzaji ana hadithi yake binafsi kuhusu enzi ya Taliban. Kwa mfano, Haji Murad Ali anayeuza keki, biskuti na vitamutamu vingine, anasema kuwa yeye aliwahi kusumbuliwa na Wataliban mara 32. "Ulikuwa ukifuatwa na Taliban ulipovaa nguo mpya tu. Hapo walidhani kuwa wewe ni kamanda ulie tajiri. Walianza kukuchapa kwa waya. Walitesa watu. Walijifurahisha kwa kumwagia mtu maji baridi. Kile walichotaka ni fedha." Anasema Haji.
Lakini je, hali ya usalama wake binafsi imekuwa bora zaidi baada ya kuondoka kwa Taliban? Hivi karibuni, Haji Murad Ali aliibiwa dukani kwake. "Polisi walikuja dukani, lakini badala ya kunisaidia, waliniambia niwasahau wezi hao. Niliibiwa kadi ya simu na bidhaa zingine dukani. Lakini ukibishana na polisi wewe utakamatwa, kwa hivyo nikaufunga mdomo wangu. Ama sivyo ningeishia jela, huko shimoni." Anabainisha Haji.
Kuna maisha mengine pia katika mtaa wa Karte Seh. Mfano ni familia ya mchanganyiko wa makabila. Sonia ni Mrusi, mume wake Sanjar ni Muafghani. Wawili hawa walikutana Poland, ambako Sanjar alikwenda kwa ajili ya masomo ya juu akisaidiwa na serikali. Sasa wanaishi karibu na jengo la bunge. "Jirani yetu ni mbunge. Alitajirika ghafla licha ya kutokea sehemu za vijijini. Mtu hujiuliza mtumishi wa serikali amepata wapi fedha hizo zote." Anasema Sanjar.
Kwa Sanjar, bunge na vita vya wenyewe kwa wenyewe mjini Kabul mwanzoni wa miaka ya 90 ni kitu kimoja. "Bunge limejaa wauaji. Watu hao ndio waliouteketeza mtaa huu. Wao wanawajibika kwa vifo vya zaidi ya watu 60,000. Safari moja walitufyatulia risasi tulipokuwa tukisafirisha gunia la ngano kwa baiskeli. Sasa wameketi bungeni. Wanashangiriwa na wanadiplomasia wa nchi za magharibi kama ishara ya demokrasia mpya. Demokrasia gani? Watu hao wanapaswa kufikishwa mahakamani."
Hamu ya kupata elimu
Ni wachache wanaobahatika kupata msaada wa serikali kusoma nchi za kigeni, kama ilivyokuwa na Sanjar. Lakini njaa ya elimu ni kubwa mno nchini humo. Wanafunzi wanagombea nafasi katika vyuo vikuu vya binafsi, kwani wanaomaliza shule ni wengi sana. Kwa muda mrefu sasa, vyuo vikuu vya serikali vinashindwa kuwachukua wanafunzi hao, kwani nafasi ni chache kuliko wale wanaotaka kujiandikisha kwa masomo zaidi.
Taasisi ya Ibn Sina ni chuo cha binafsi kilichopewa jina la msomi maarufu wa Kiislamu na kiasi ya wanafunzi 300 wamejiandikisha huko. Ali Amiri aliyesomea falsafa ya mwanafilosofia Wittgenstein, yupo katika bodi ya wakurugenzi ya taasisi hiyo. Yeye anaamini kuwa taasisi yake inaunga mkono mageuzi. "Kwa muda mrefu Wahazara walio wachache walikuwa wakibaguliwa. Kwa mfano, hawakuruhusiwa kuwa maafisa jeshini au kusomea sheria na siasa. Marufuku hiyo imeondoshwa na sasa wanafunzi wanachukua masomo hayo." Wanafunzi wa kike wanapunguziwa sehemu ya malipo. Wakati wa utawala wa Taliban, inasemekana wanawake walizuiwa kupata elimu yoyote ya Kimagharibi kwa maelezo kuwa ni haramu kwao.
Darasani zaidi ya nusu ya wanafunzi ni wanawake. Wanaume hutengwa na hukaa mistari ya nyuma. Wanawake hujifunika vichwa na baadhi yao wamejipodoa. "Unachoona hapa hukutikana huku Kabul tu. Huku ndio mwanamke huweza kujifunika kichwa kama apendavyo. Wanasoma kujiendeleza zaidi. Katika maeneo ya vijijini, mwanamke hawezi kutoka nyumbani peke yake wala kwenda kusoma. Akitoka, basi lazima avae baibui la kumfunika mwili mzima." Anasema mmoja wa wanafunzi wanawake wanaochukua masomo ya juu. Mwanafunzi huyu anaongezea kuwa, kazi ya wanawake vijijini ni kufua na kusafisha nyumba. Kwa wanaume wa sehemu hizo, mwanamke ni kama chombo cha uzazi. Katika maeneo hayo, kuna wanawake wanaozaa hadi watoto 18. "Hali hii inatisha sana". Anasema mwanafunzi huyo.
Hata hivyo, wengi wa wanawake hawa wanaosoma sasa wanasema hawataki kujiingiza kwenye mambo ya siasa, ambako labda wangeliweza kubadilisha hali ya mamabo, na sababu ni kuwa wamepoteza imani na wasiasa. "Mimi sitaki kuwa mbunge. Hiyo huleta matatizo tu. Mtu hulazimishwa kufanya mambo yasio ya kibinadamu. Mimi nasomea sheria kwani nataka kugombea haki za wanawake wanaokandamizwa." Anasema mwanafunzi mwengine wa kike.
Mwandishi: Martin Gerner/ZPR
Tafsiri: Prema Martin