1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maendeleo yafikiwa kuzuwiya malaria.

Mohamed Dahman18 Oktoba 2007

Watoto wengi zaidi wa Afrika wamekuwa wakipata majumbani mwao vyandarua vya kulalia vilivyochovywa madawa ya kutokomeza mbu na wengine wengi zaidi wamekuwa wakitibiwa kwa malaria.

Mbu wa kuambukiza malaria.
Mbu wa kuambukiza malaria.Picha: DW-TV

Umoja wa Mataifa na wataalamu wa afya ya watoto katika repoti iliotolewa hapo Jumaatano wanaeleza maendeleo yaliofikiwa kuzuwiya malaria.

Wamesema hizo ni habari njema kuhusu malaria kuwahi kutolewa kwa miongo mingi lakini wamesema vyandaruwa hivyo bado vimekuwa vikitolewa kwenye nchi chache na watu wengi walioko hatarini kuathirika na malaria wamekuwa hawapati matibabu mazuri kwa ugonjwa huo unaosababishwa na mbu ambao huuwa watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja kila mwaka.

Repoti hiyo kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Watoto UNICEF inasema kwa mara ya kwanza hivi sasa wameweza kurepoti juu ya kuboreka kwa hatua za kinga kwa ajili ya kudhibiti malaria kama vile matumizi ya vyandaruwa vililivyochovywa madawa ya kuulia mbu.

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Ann Veneman amewaambia waandishi wa habari kwamba mchango wa fedha kwa ajili ya kudhibiti malaria umeongezeka kwa zaidi ya mara 10 katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.Amesema idadi ya vyandaruwa vilivyochovywa madawa vinavyozalishwa duniani vimeongezeka zaidi ya maradufu kutoka milioni 30 hapo mwaka 2004 na kufikia milioni 63 hapo mwaka 2006.

Hata hivyo repoti hiyo inasema kwamba vyandaruwa viliochovywa madawa milioni 264 vinahitajika kuwahifadhi asilimia 80 ya wanawake wajawazito na watoto wenye umri wa miaka mitano ambao wako kwenye hatari ya kupata malaria barani Afrika.

Repoti hiyo pia inataja maendeleo yaliofikiwa katika kutibu malaria ambapo nchi nyingi zaidi zinatumia madawa yaliopendekezwa na Shirika la Afya Duniani kwa ajili ya kutibu malaria.

Madawa ya zamani yamekuwa hayafanyi kazi tena dhidi ya ya virusi vingi vinavyoambukizwa na mbu lakini tiba mpya zenye kuzingatia madawa yanayoitwa artemisinins yamekuwa mjarabu iwapo wagonjwa wanaweza kuyapata.

Ikitaja baadhi ya miradi ya mafanikio repoti hiyo inataja mfano wa Kenya ambapo zaidi ya vyandaruwa milioni 10 vilivyotiwa madawa vimesambazwa nchini humo tokea mwaka 2003 na kwamba kwa kila kundi la watoto 1,000 nchini humo wanaolala kwa kutumia vyandaruwa hivyo vifo vya watoto watano au sita vinaweza kuzuilika.

Vyandaruwa hivyo 230,000 vimesambazwa kwenye visiwa vya Zanzibar nchini Tanzania ambapo maafisa wa afvya visiwani humo wameripoti kupunguwa kwa asilimia 87 kesi za malaria kwenye kisiwa cha Pemba kutoka kesi 12,000 hapo mwaka 2002 hadi kuwa kesi 1,500 hapo mwaka 2006.

Kati ya matukio milioni 350 na milioni 500 ya malaria hutokea kila mwaka na kupelekea vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia milioni moja wengi wao katika eneo la kusini mwa jangwa la Sahara barani Afrika na miongoni mwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano.

Malaria pia huchangia utapiamlo ambayo ni sababu ya vifo kwa zaidi ya nusu ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO kazi ya kutafuta chanjo ya ugonjwa huo inaendelea lakini njia bora ya kuzuwiya maambukizo ya malaria ni kwa kutumia vyandaruwa vilivyochovywa madawa ya kuuwa mbu.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW