1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiAsia

Mafuriko Indonesia vifo vyaongezeka

Zainab Aziz DPA/RTRE
27 Novemba 2025

Mamlaka katika kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia zimesema idadi ya vifo kutokana na mafuriko na maporomoko ya ardhi imeongezeka hadi watu zaidi ya 60 na wengine zaidi ya 50 hawajulikani walipo.

Indonesia Padang 2025 | Shughuli za uokozi kaskazini mwa kisiwa cha Sumatra
Eneo la Padang kaskazini mwa kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia lililoathiriwa na mvua kubwa na maporomoko ya ardhiPicha: Ade Yuandha/AFP/Getty Images

Maafa hayo yametokea baada ya mafuriko na maporomoko ya ardhi kulikumba jimbo la Sumatra lililopo Kaskazini mwa Indonesia kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa siku kadhaa.

Msemaji wa polisi wa mkoa  wa Sumatra amefahamisha kuwa viwango vya maji katika baadhi ya maeneo vimefikia kina cha juu ya mita moja.

Kulingana na data za polisi, matukio 148 ya maafa yameorodheshwa tangu Novemba 24 katika wilaya na miji 12.  Maafa hayo ni pamoja na maporomoko ya ardhi 86, mafuriko 53, miti kadhaa iliyoanguka na matukio mawili ya kimbunga.

Waokoaji wanaendelea na shughuli za kuwakoa wakazi waliokwama kwenye maji yenye matope yanayotiririka kwa kasi ambayo yameingia majumbani na kuwalazimisha maelfu ya watu kukimbia makazi yako pia kwa hofu ya kuzuka kimbunga katika kisiwa cha Sumatra.

Waokoaji wakiendelea kuwaokoa watu kutoka kwenye maafa ya mafuriko huko Sumatra nchini IndonesiaPicha: Basarnas/Anadolu Agency/IMAGO

Idara ya hali ya hewa imesema kutokana na hali mbaya ya hewa, mafuriko zaidi yanatarajiwa katika majimbo mengine kadhaa ya Sumatra ya Aceh na Riau, katika siku mbili zijazo.

Kwa mujibu wa afisa katika shirika la kukabiliana na maafa huko Sumatra Kaskazini, mawasiliano na nguvu za umeme vimekatwa, na sehemu kubwa katika maeneo yaliyoathirwa haiwezi kufikiwa. Afisa huyo ameeleza kuwa watu wapatao elfu kumi na mbili wamehamishwa na wengine wengi bado wanasubiri msaada katika majimbo kadhaa kwenye kisiwa hicho cha Sumatra.

Maafisa wa kukabiliana na maafa katika eneo hilo la magharibi mwa kisiwa cha Sumatra wameelezea hofu kwamba idadi ya vifo huenda ikaongezeka kutokana na daraja lililoangushwa na mvua inayoendelea kunyesha.

Mkuu wa serikali ya mtaa wa eneo la kati Tapanuli amelaumu ukataji haramu wa miti na ukataji miti kwa ajili ya mashamba ya matunda ya michikichi kuwa ndio umezidisha mafuriko na maporomoko ya ardhi. Indonesia ndio mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya michikichi duniani.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW