Mafuriko Libya: Idadi ya vifo huenda ikafikia 20,000
14 Septemba 2023Kiongozi huyo ameyasema hayo alipokuwa akihojiwa na kituo cha runinga al-Arabiya TV siku ya Jumatano.
Al Ghaithi amesema idadi hiyo huenda ikafikiwa kutokana na jumla ya watu ambao hadi sasa haijulikani waliko. Mafuriko hayo nchini Libya yamekwishasababisha vifo vya watu wasiopungua 5,200, na maelfu ya wengine wakijeruhiwa. Hadi sasa watu 10,000 ndio kimsingi hawajulikani waliko. Mataifa mbalimbali yameendelea kutuma misaada kwa Libya.
Soma pia: Ujerumani,Romani na Finland zapeleka msaada nchini Libya
Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) limesema karibu watu 30,000 wameyahama makazi yao huko Derna huku maelfu ya wengine wakipoteza kabisa makazi yao katika miji ya mashariki mwa nchi hiyo. Kulingana na Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 300,000 wameathiriwa na mafuriko hayo.
Shirika la misaada la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) limesema siku ya Jumatano kuwa litaagiza kikosi cha dharura nchini Libya. Kikosi hicho kinacho wajumuisha wataalamu wa matumizi ya vifaa mbalimbali na wahudumu wa afya, kinatarajiwa kuwasili Alhamisi mjini Derna ili kutathmini mahitaji ya kiafya.
Mzozo wa kisiasa Libya
Serikali mbili hasimu zinagombea madaraka nchini Libya, ambayo imekuwa ikikumbwa na machafuko katika miaka ya hivi karibuni. Serikali moja ina makao yake mashariki na nyingine mjini magharibi mwa nchi katika mji mkuu, Tripoli.
Soma pia: Zaidi ya watu 3,000 waliokufa kwa mafuriko Libya wamezikwa
Hadi sasa, juhudi za kidiplomasia za kutafutia suluhu ya amani kwa mzozo huo wa vita vya wenyewe kwa wenyewe zimekuwa zikigonga mwamba. Libya imekuwa katika machafuko tangu kupinduliwa kwa rais Moamer Gaddafi mwaka 2011.
Wanamgambo wasiohesabika bado wanapigania madaraka na ushawishi katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. Na mzozo huo kwa kiasi kikubwa unachochewa zaidi na mataifa ya kigeni.
(DPAE,RTRE)