1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha maelfu kukosa makazi Burundi

22 Aprili 2024

Zaidi ya wakaazi 2,400 katika kijiji cha Gabaniro nchini Burundi wameachwa bila makaazi baada ya kutokea maporomoko ya udongo kutoka kwenye mlima uliokuwa karibu na kijiji hicho na kuzibomoa zaidi ya nyumba 400.

Burundi -mafuriko-Gatumba
Mafuriko yaliyoukumba mji wa Gatumba karibu na Bujumbura mwaka 2021Picha: Antéditeste Niragira/DW

Hayo yanajiri wakati ambapo tayari ofisi zinazohusika na masuala ya kwenye mpaka wa Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zikiwa zimefurika baada ya maji kujaa katika katika Ziwa Tanganyika na kusimamisha huduma ya usafiri wa raia kutoka na kuingia katika nchi hizo mbili ambao wanatumia njia ya barabara.

Soma: Burundi yahitaji msaada kukabiliana na mafuriko makubwa

Raia wa kijiji cha Gabaniro tarafani Gitaza katika mkoa wa Rumonge kusini mwa nchi, wameeleza kuwa wameshuhudia mlima uliokuwa katika na kijiji hicho unavyoporomoka.

Mafuriko yaliyoikumba Burundi 2021Picha: Antéditeste Niragira/DW

Unapowasili kwenye eneo hilo utashuhudia kijiji hicho cha Gabaniro kimesalia wazi kwani hakuna nyumba hata moja iliyonusurika katika maporomoko hayo.

Waliokuwa wakaazi wa kijiji hicho wanasema walianza kuona nyufa nyingi kwenye nyumba zao tangu siku ya Ijumaa na kuanza kuokoa vitu kabla ya janga hilo kutokea.Burundi yaomba msaada wa haraka kufuatia mafuriko

Mshauri wa gavana wa mkoa huo wa Rumonge, Abdoul Ntiranyibagira anasema hadi sasa wameorodhesha kifo kimoja ambacho ni cha mtoto wa miaka minne ambaye amekufa, huku watu wengine kadhaa wakiwa wamejeruhiwa wakati wakikimbia janga hilo.

''Matokeo ya haraka tulionayo ni mtu mmoja ameuwawa na wengine wanne wamejeruhiwa. Pia nyumba 407 zimebomoka, walikokuwa wakiishi watu 2,485, ambao kwa sasa wamebaki bila makaazi. Mashamba yenye ukubwa wa heka zaidi ya 500 yameharibika na mazao yaliyokuwa yanatarajiwa kuvunwa siku za usoni. Pia kuna miundombinu ya umma iiyoteketea katika maporomoko hayo, bwawa la mradi wa kuendeleza umeme Kirasa, limetoweka kabisa majengo na vifaa vyote vilivyokuwa katika mradi huo vimeharibika,'' alisema mshauri wa gavana.

Raia hao waliopoteza makaazi yao wamekusanywa kwa sasa na wanahifadhiwa katika shule ya kiufundi.

Maporomoko hayo ya udongo yametokea siku moja baada ya baraza la mawaziri kutangaza wakaazi wa Gatumba maeneo yanaokaribia mpaka wa Burundi na Kongo wataanza kuondolewa na kuhamishiwa Kabezi mkoani Bujumbura vijijini, ambapo maji ya Ziwa Tanganyika yanazidi kuongezeka. Tayari ofisi za uhamiaji zimefunikwa na maji na kusitisha usafiri wa raia katika nchi hizi mbili kupitia barabara.

Mafuriko yaharibu miundombinu ya barabara Kongo- Burundi

02:42

This browser does not support the video element.

Hali kadhalika katika tarafa ya Buganda mkoani Cibitoke magharibi mwa Burundi kunatuwama maji yaliyoanza kuonekana katika mashamba.

Mhadhiri kwenye chuo kikuu cha Burundi Athanase Nkuzimana ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya mazingira amewataka raia wanaoishi kwenye maeneo yaliyo karibu na milima kuondoka.Maelfu waachwa bila makao kufuatia mafuriko Burundi

''Kinachoshuhudiwa ni maporomoko ya ardhi, maeneo ya milimani yanaachana. Sababu ni nyingi aidha aina ya ardhi ama mlima ulio mrefu kwenye kijiji. Kwa kusubiri hatua zinazohitajika ni muhimu wakaazi wa maeneo hayo waondoke.''

Burundi imetajwa kuwa miongoni mwa nchi 20 zinazokabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi. Tayari serikali ilitowa wito kwa jumuiya ya kimaitaifa kusaidia ili iweze kuwahudumia waathiriwa wa majanga hao ya kimaumbile. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW