1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yasababisha vifo New York

3 Septemba 2021

Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza hali ya dharura kwenye majimbo ya New York na New Jersey na kuagiza wahanga wa mafuriko yaliyokumba maeneo hayo kupewa misaada.

USA Hurricane Ida Wirbelsturm George County
Picha: Hannah Ruhoff/The Sun Herald/picture alliance/AP

Rais Joe Biden wa Marekani ametangaza hali ya dharura katika majimbo ya New York na New Jersey na kuagiza taasisi za serikali ya shirikisho za kupambana na majanga kuratibu juhudi za kuwasaidia wahanga na kutoa misaada ya dharura kwa wahanga wa mafuriko. Taarifa zinasema takriban watu 45 wamekufa kwenye mafuriko hayo. 

Rais Joe Biden ametangaza hali hiyo ya dharura kabla ya ziara yake katika jimbo la Lousiana ambako hapo kabla kimbunga Ida kiliharibu majengo na kuwaacha wakazi zaidi ya milioni moja kwenye giza baada ya umeme kukatika.   

"Ujumbe wangu kwa wote walioathirika ni kuwa tuko pamoja katika hili. Taifa litawasaidia. Huo ndio ujumbe nilioutoa kwa mameya, magavana na viongozi wa taasisi za nishati kwenye eneo hilo, ambao wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na utawala wangu katika siku chache zilizopita." alisema Biden.

Ndio ujumbe wa rais Biden alipolihutubia taifa kuhusiana na majanga ya kiasili yanayolikumba taifa hilo, na hasa baada ya kimbunga Ida kilichofuatiwa na mafuriko mabaya kabisa kaskazini mashariki mwa Marekani.

Ametumia pia fursa hiyo kuwakumbusha raia kwamba majanga kama kimbunga hicho cha Lousiana, mafuriko na mioto huko California na Nevada kwa pamoja yanachangiwa na mabadiliko ya tabianchi na kwa maana hiyo wote kwa pamoja wanatakiwa kuchukua hatua kuzuia ongezeko la joto ulimwenguni.

Soma Zaidi. Maoni: Lazima tuchukue hatua sasa kuhusu tabia nchi

Mitaa ya New York imefurika maji na vikosi vya uokozi vimeendelea kuwasaidia wahanga wa mafuriko baada ya kimbunga Ida.Picha: Mike Segar/REUTERS

Mitaa ya New York imegeuka mito kutokana na kufurika maji na njia za chini ya ardhi zimefungwa kutokana na kina cha maji kuongezeka na kuziba reli. Mmiliki mmoja wa mkahawa wa Manhattan Metodija Mihajlov amesema hajawahi kushuhudia mvua kubwa kama hiyo. Safari nyingi za ndege zimeahirishwa katika viwanja vya LaGuardia na JFK pamoja na Newark ambako video zinaonyesha njia ya kuondokea ndege imefurika maji.

Gavana wa New Jersey Phil Murphy amewaambia waandishi wa habari kwamba karibu watu 23 wamekufa jimboni mwake, na vifo vingi vilitokea baada ya magari kusombwa na mafuriko. Watu 13 wamekufa katika jiji la New York, ikiwa ni pamoja na 11 walioshindwa kutoka kwenye makazi yao yaliyopo chini ya ardhi.

Tizama Video: 

Biden anatarajiwa kukutana na gavana wa Lousiana John Bel Edwards na maafisa wa eneo hilo na kuzuru  eneo jirani la LaPlace ambalo pia limeathirika pakubwa na maeneo mengine.

Wanasayansi wanasema mabadiliko ya tabianchi yanachangia ongezeko la matukio mabaya kabisa ya hali ya hewa kama dhoruba kali za tropiki, na ukame pamoja na joto kali linalochochea mioto ya msituni. Maafisa wa taasisi ya hali ya hewa nchini Marekani waliripoti kwamba Julai ya mwaka huu, ulikuwa mwezi wenye joto kali zaidi kuwahi kurekodiwa katika kipindi cha miaka 142.

Soma Zaidi: Kimbunga Ida chapungua kasi Marekani

Mashirika: APE/AFPE