1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuriko yatishia kupindukia yale mwaka 2002

4 Juni 2013

Kansela Angela Merkel ameyatembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko makubwa kusini na mashariki ya Ujerumani katika wakati ambapo kima cha maji kinazidi kupanda katika baadhi ya maeneo ya Ulaya ya kati .

Kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer wakiutembelea mji wa PassauPicha: Reuters

Hali bado ni ya wasi wasi nchini Ujerumani,jamhuri ya Tcheki ambako mtu wa nane amegunduliwa amekufa ,pamoja pia na Austria,walikokufa watu wawili,Uswisi mtu mmoja na Hungary.

Kote huko mafuriko yamesababisha maafa na hasara kubwa na maelfu ya watu kulazimika kuzihama nyumba zao.

Kansela Angela Merkel, akivalia koti jeusi na viatu vya mvua,aliutembelea mji wa Passau,katika jimbo la kusini la Bavaria,mmojawapo ya miji iliyoathirika zaidi na mafuriko hayo.Kansela Angela Merkel ameahidi msaada wa dharura wa Euro milioni 100 kuyasaidia maeneo yaliyoathirika.Kansela Angela Merkel amesema:

Kansela Angela Merkel amepanga kuitembelea miji mengine pia iliyoathirika katika jimbo la Saxony na Thüringen ambako kima cha maji kinazidi kupanda.Wanajeshi elfu nne wamepelekwa kusaidia.

Duru zinasema hata hivyo katika mji wa Passau ambako maji ya mito mitatu inamwaagikia katika mto Danube,kima cha maji kimeanza kushuka.

Bado hali si shuwari

Magunia ya amchanga yamewekwa kuzuwia maji yasiingie ndani ya nyumba karibu na mto Elbe mashariki ya UjerumaniPicha: JOHANNES EISELE/AFP/Getty Images

Mjini Prague,maji ya mto Valtva yamefikia kilele chake i na maji yanaayofurika yanaelekea kaskazini ya jamhuri ya Tcheki.

Wasi wasi mkubwa zaidi ni katika mji wa Usti-nad-Labern,mji wa kiviwanda wenye wakaazi laki moja unaokutikana karibu na mto Elbe,kilomita 30 karibu na mpaka wa Ujerumani.

Viwanda vya kemia katika eneo hilo vimefungwa,viongozi wakihofia waasije wakashuhudia balaa kama lile lililotokea katika mafuriko ya mwaka 2002 .

Nchini Austria kima cha maji ya mto Danube kinatarajiwa kupanda wakati wowote ule na kufikia kiwango sawa na kile cha mafuriko ya mwaka 2002.

Nchini Hungary waziri mkuu Viktor Urban ametangaza hali ya hatari katika baadhi ya majimbo kutokana na kuzidi kupanda kima cha maji ya mto Danube.Na huko pia wanajeshi elfu nane pamoja na maelfu ya waokozi na askari polisi wamepelekwa katika maeneo ya maafa.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/AP

Mhariri:Mohamed Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW