Mafuriko yaua watu 14 Kenya, familia elfu 15 zaathirika
6 Novemba 2023Kulingana na shirika la msalaba mwekundu maelfu wameachwa bila makao huku ikikadiria hasara kubwa zaidi mvua hiyo inapoendelea kunyesha.
Mgogoro wa kibinadamu huenda ukashuhudiwa kutokana na athari za mafuriko yanayoshuhudiwa nchini Kenya hasa maeneo ya pwani, Kaskazini Mashariki, bonde la ufa na magharibi mwa nchi.
Kulingana na shirika la msalaba mwekundu, zaidi ya familia elfu 15 zimeathiriwa, mifugo zaidi ya elfu moja wamefariki, na mazao ya mashamba kiasi cha heka 241 yameharibiwa na mafuriko.
Soma pia:Wokoaji wanapambana kufikia wahanga wa mafuriko India
Mbunge wa Nyandarua Faith Gitau aamesema miongoni mwa madhara yaliosababishwa na mvua hizo ni pamoja na mazao kuoza shambani na miundombinu ya usafiri kuharibika vibaya.
"Tunahitaji watu watathmini waje wakague ili kujua namna gani maji yaha yataelekezwa kwenye mkondo wake." Alisema.
Hali ya miundombinu yatatiza mawasiliano
Mafuriko yamesababisha kukatika kwa madaraja, barabara zikifurika kiasi cha kutopitika na hivyo kutatiza huduma muhimu kama vile uchukuzi wa vyakula, mitihani ya kitaifa inayoendelea, na wagonjwa kufikia vituo vya afya.
Viongozi kutoka maeneo ya kaskazini mashariki wanataka hali hii ya mafuriko itangazwe kuwa janga la kitaifa huku wakiomba msaada wa mahitaji muhimu.
Idara ya utabiri wa hewa nchini Kenyaimesema mvua kubwa itaendelea kunyesha ikiandamana na radi kwenye baadhi ya maeneo.
Kuna wasiwasi wa mlipuko wa magonjwa yanayotokana na maji, kufuatia kufurika na kusombwa kwa vyoo.
Amos Mariba Kamishna wa kaunti ya Mandera anawahimiza wakaazi kuzingatia usalama wao wakati huu.
Katika baadhi ya maeneo athirika ndege aina ya helikopta zimetumika kuwaokoa watu na kusambaza mitihani kwa watahiniwa wanaoendelea na mitihani ya kitaifa.