Mafuriko yazikumba nchi kadha za kusini mwa Afrika.
8 Januari 2008Lusaka.Kiasi cha watu milioni 1.5 nchini Zambia huenda wakazihama nyumba zao kutokana na mafuriko yanayolikumba eneo la kusini mwa Afrika ambayo yamesababisha maeneo kadha ya Zimbabwe kutofikika na kuuwa watu sita nchini Msumbiji.Televisheni ya taifa ya Zambia imeonyesha watu wakiwa wamebeba vitanda, kuku na mbuzi vichwani wakati wakiondoka kutoka maeneo hayo wakipita katika maji. Nusu ya nchi hiyo imo katika hali ya tahadhari.
Mamia ya watu wako katika hatari katika eneo hilo baada ya mvua kubwa , umesema umoja wa mataifa ambao unaishauri serikali kutathmini uharibifu uliofanywa na mafuriko hayo.
Mafuriko nchini Zimbabwe , nchi ambayo inakabiliwa na mzozo wa kiuchumi pamoja na ukosefu wa chakula na mafuta, yameharibu miundo mbinu na kuzuwia mawasiliano na maeneo makubwa ya nchi hiyo.