1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mafuta yapanda bei baada ya mkutano wa OPEC kuvunjika

Josephat Charo
6 Julai 2021

Bei ya mafuta imeendelea kupanda katika masoko ya barani Asia baada ya mkutano wa nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani OPEC kuvunjika bila makubaliano juu ya mpango ulionuiwa kuongeza uzalishaji.

Symbolbild OPEC, Organisation Erdöl exportierender Länder
Picha: picture-alliance/dpa/B. Gindl

Kuvunjika kwa mazungumzo kati ya mataifa wanachama wa OPEC na wadau wengine kumeongeza uwezekano wa mafuta kufikia bei ya dola 100 kwa pipa, kiwango ambacho hakijawahi kuonekana tangu mwaka 2014. Hali hii imeibua hofu kuhusu mfumuko wa bei, ambao yumkini ukazilamisha benki kuu kubadili sera zao za kufanya miamala ya fedha au kuongeza viwango vya riba mapema kuliko ilivyokuwa imepangwa hapo kabla.

Masoko ya hisa barani Asia yameonekana yakiyumba huku likizo fupi ya siku ya uhuru ya Marekani siku ya Jumatatu ikiwa na maana hakukuwa na vichocheo vingi vya ununuzi wa hisa. Masoko ya hisa ya Tokyo, Singapore, Seoul, Mumbai, Bangkok na Jakarta yote yameshuhudia thamani ikipanda, lakini masoko ya Shanghai, Sydney, Wellington, Taipei na Manila yameporomoka. Thamani ya hisa katika masoko ya hisa ya London, Paris na Frankfurt iliporomoka muda mfupi baada ya kufunguliwa kwa ajili ya biasahra.

Makampuni ya teknolojia katika kisiwa cha Hong Kong yamebaki katika hali ya wasiwasi kutokana na hofu ya ukandamizaji mpya kwa sekta hiyo na maafisa wa China ambao utazifanya hisa zisiwavutie wawekezaji.

Nchi wanachama wa OPEC na wadau wengine walifuta mkutano wao siku ya Jumatatu ulionuiwa kutafutia ufumbuzi mkwamo kati ya Falme za Kiarabu na wanachama wengine kuhusu jinsi ya kuongeza utoaji na usafirishaji mafuta. Hakuna tarehe mpya ya mkutano iliyotangazwa.

Saudi Arabai yaukosoa Umoja wa Falme ua Kiarabu

Waziri wa nishati wa Saudi Arabia Abdulaziz bin Salman ameukosoa msimamo wa Umoja wa Falme za Kiarabu kupinga makubaliano ya OPEC na wadau wengine. "Juhudi kubwa zimefanywa katika kipindi cha miezi 14 iliyopita zilizosaidia kuleta tija na matokeo mazuri sana. Na itakuwa aibu kutoyaendeleza mafanikio hayo. Makubaliano na uzalendo fulani ndiyo mambo yatakayotuokoa," aliongeza waziri huyo.

Waziri Abdulaziz bin SalmanPicha: AFP/J. Klamar

Nchi za OPEC zimekuwa zikiongeza kiwango cha mafuta katika miezi ya hivi karibuni baada ya kupunguza mwaka uliopita, kukabiliana na kuporomoka  bei za mafuta kulikosababishwa na janga la corona. Kutokana na mahitaji kuongezeka kwa kasi kwa sababu ya uchumi kuanza kufufuka tena, na kukaribia kwa msimu wa likizo nchini Marekani, maafisa walipanga kuongeza uzalishaji mafuta hadi mapipa 400,000 kwa siku kila mwezi kuanzia mwezi Agosti hadi Desemba, lakini mkwamo uliojitokeza una maana njia mpya za kukidhi mahitaji zitahitajika.

Lakini huku bei za mafuta zikiongezeka kwa kasi, wachambuzi wanasema kukosekana makubaliano ina maana hakutakuwa na ongezeko la uzalishaji na hivyo bei za mafuta zitaendelea kupanda. Kwa upande mwingine migogoro ndani ya OPEC inaweza kuisambaratisha jumuiya hiyo huku nchi wanachama zikigombania masoko kwa kupunguza bei.

Warren Patterson wa shirika la kimataifa la benki na huduma za miamala ya fedha la Uholanzi, ING Group NV amesema kushindwa kwa OPEC na nchi nyingine wadau kukubaliana kutaongeza hali ya wasiwasi katika masoko ya mafuta. Patterson aidha amesema iwapo hakutapatikana suluhisho la haraka, wasiwasi kuhusu uzalishaji mafuta wa jumuiya ya OPEC katika miezi ijayo kunaashiria masoko yatayumba zaidi kwa kiwango kikubwa.

(afpe)