Magaidi wauwa raia 100 Burkina Faso
5 Juni 2021Kwa mujibu wa maafisa wa usalama na wenyeji wa eneo yalikotokea mauaji hayo, mashambulizi yalifanyika usiku wa Ijumaa (Juni 4) kuamkia Jumamosi (Juni 5), wakati watu wenye silaha walipoanzisha uasi kwenye mji wa kaskazini wa Solhan.
Msemaji wa serikali, Ousseni Tamboura, alisema kwenye taarifa yake kwa vyombo vya habari kwamba soko pamoja na nyumba kadhaa zilichomwa moto katika jimbo hilo la Yagha lililo karibu na mpaka wa nchi hiyo na Niger.
Akitangaza masaa 72 ya maomboleza, Rais Roch Marc Christian Kabore wa Burkina Faso aliyalaani mashambulizi hayo aliyoyaita ya kinyama.
Mwenyeji mmoja ambaye alikataa kutajwa jina akihofia usalama wake na ambaye aliwatembelea majeruhi wa mashambulizi hayo, alisema aliwaona watu 12 kwenye chumba kimoja na wengine kumi kwenye chumba chengine.
"Kulikuwa na jamaa wengi wakiwashughulikia majeruhi. Kulikuwa na watu wengine wengi pia wakikimbia Solhan kukimbilia Sebba... Watu wanaogopa," aliliambia shirika la habari la AFP.
Kwa mujibu wa afisa mmoja wa usalama, washambuliaji walikivamia kikosi cha sungusungu kiitwacho VDP kinacholisaidia jeshi kupambana na magaidi majira ya saa nane usiku, kabla ya kuyavamia majumba ya raia na kufanya mauaji.
Kikosi hicho cha VDP kilianzishwa mwezi Disemba 2019 kulisaidia jeshi lenye vifaa duni la Burkina Faso kupambana na magaidi, lakini hadi sasa chenyewe kimeshapoteza wapiganaji zaidi ya 200, kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa na shirika la habari la AFP.
Magaidi waigeukia Burkina Faso
Hayo ni mashambulizi mabaya kabisa kuwahi kufanyika nchini Burkina Faso tangu taifa hilo la Afrika Magharibi kuvamiwa na makundi ya wapiganaji wa itikadi kali wenye mafungamano na makundi ya kigaidi ya al-Qaida na lile lijiitalo "Dola la Kiislamu."
Mtafiti wa ngazi za juu wa taasisi inayojihusisha na ukusanyaji takwimu za mapigano na maeneo yanakotokea mapigano hayo, Heni Nsaibia, ameliambia shirika la habari la AP kwamba sasa ilikuwa wazi "makundi ya wanamgambo yameiweka Burkina Faso kuwa uwanja wao wa mapambano."
Licha ya kuwepo kikosi maalum cha mataifa ya Sahel na pia Ufaransa kutuma wanajeshi wake 5,000 kwenye eneo hilo, mashambulizi ya makundi ya itikadi kadi yanazidi kushamiri.
Katika kipindi cha wiki moja tu mnamo mwezi Aprili, zaidi ya watu 50 waliuawa nchini Burkina Faso, wakiwemo waandishi habari wawili wa Uhispania na mtunza mazingira mmoja kutoka Ireland.
Zaidi ya watu 1,300 wameshauawa na wengine milioni moja kulazimika kuwa wakimbizi wa ndani wakikimbia mauaji na mashambulizi ya makundi hayo nchini humo.