Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika
3 Machi 2023Süddeutsche Zeitung
Limeandika juu ya ziara ya Macron Afrika kwa kuanza kunukuu kauli ya rais huyo wa Ufaransa akisema Afrika sio tena banda la uwani la Ufaransa. Rais Macron ameshasafiri barani Afrika sio chini ya mara 14 na pengine hata zaidi, kwa mujibu wa taarifa kutoka kasri ya Elysee. Lakini ziara iliyoanza siku ya Jumatano wiki hii ilitajwa kuwa ziara muhimu zaidi ya rais huyo wa Ufaransa katika nchi nne za bara hilo la Afrika,Gabun, Angola, Jamhuri ya Kongo-Brazaville na Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo.Muhariri anaendelea kusema kwamba ziara hiyo ya Macron imekuja wakati muhimu sana, kipindi ambacho Ufaransa inatafakari dhima yake katika bara hilo na kwahivyo ni wakati muhimu katika kihistoria ya uhusiano na bara la Afrika.Ni wakati ambapo nchi hiyo imeamua kuifikisha mwisho sera ya mwelekeo zaidi wa kijeshi katika bara hilo.Lakini pia mhariri anakumbusha kwamba ushawishi wa Ufaransa katika nchi zilizokuwa makoloni yake barani Afrika unayumba,na makundi ya harakati ya kuipinga Ufaransa yanaongezeka katika ukanda wa Sahel. Mhariri pia amekwenda mbali zaidi na kuuliza ni nani atakayejaza pengo linaloachwa na Ufaransa. Bila shaka suali hili sio gumu kiasi hicho kulijibu. China na Urusi ambazo zimekuwa zikitetea maslahi yao katika nchi zenye rasilimali hivi sasa zimezidi kujisogeza kwenye bara hilo. Anamalizia kwa kusema haijawahi kutokea ushawishi wa Ufaransa kuwa katika hali dhaifu kama ilivyo sasa na nchi hiyo imepata washindani wa wazi.
Handelsblatt
Limeandika kwamba mtazamo wake juu ya uhusiano wa Ufaransa na Afrika kwa kuuliza Je rais wa Urusi Vladmir Putin anaweza kufaidika na mkakati wa Ufaransa barani Afrika. Linasema Urusi inatanua zaidi nafasi yake barani Afrika lakini kwa upande mwingine rais Emmanuel Macron anachukua hatua ya kupunguza wanajeshi wa nchi yake kutoka barani humo,kwa maneno mengine Macron amechagua mwelekeo mpya katika bara la Afrika.nNa kabla ya kuanza ziara yake kuelekea Gabon na nchi nyingine makoloni yake ya zamani barani humo,aliweka wazi kwamba Ufaransa inataka kujenga mahusiano yenye usawa na yenye kuwajibika na bara hilo. Lakini mhariri wa hilo la Handelsblatt anasema mwelekeo mpya wa Rais Macron barani Afrika unaakinisi namna ambavyo ushawishi wa nchi yake umeshapoteza nguvu katika bara hilo. Mhariri anakumbusha kwamba nchi hiyo imeyaondowa majeshi yake yaliyokuwa yakiendesha operesheni ya kulinda usalama katika nchi mbali mbali za bara hilo kuanzia Mali,Jamhuri ya Afrika ya Kati mpaka BurkinaFaso. Mhariri pia amemnukuu mtaalamu wa masuala ya Afrika kutoka taasisi moja mjini Paris akisema Operesheni iliyoshindwa ya Ufaransa ya kupambana na magaidi katika eneo la Sahel iliipa uhalali Ufaransa kuweka majeshi yake katika bara zima la Afrika. Na kwahivyo mhariri anasema suala hili linaiharibia kwa kiasi kikubwa Ufaransa kisiasa na sio hivyo tu lakini sifa ya nchi hiyo imeharibika wakati mbaya kabisa. Wakati ambao kuna ushindani mkubwa wa kimkakati barani Afrika.Mhariri anaamini kwahivyo mwisho wa siku ni mtu mmoja tu anayeweza kufaidika na makosa haya ya Ufaransa-nae ni Rais wa Urusi Vladmir Putin. Lakini pia China ina malengo makubwa katika bara hilo.
Frankfurter Allgemeine
Gazeti hilo pia limetuwama kwenye ziara ya Macron barani Afrika kwa kutangulia kusema kwamba Macron kwahakika ni rais wa kwanza wa Ufaransa aliyezaliwa baada ya enzi ya Ukoloni wa nchi hiyo barani Afrika. Na hivi sasa anataka kujitenga na urithi huo wa ukoloni alioukuta. Mhariri anasema kauli ya rais Macron kuhusu mustakabali wa mahusiano yake na Afrika imeonesha wazi kwamba anataka kuanza ukurasa mpya na bara hilo.Rais Macron amewahakikishia waafrika kwamba,kambi za kijeshi za Ufaransa zitakuwa historia katika bara hilo.
taz, die tageszeitung
Limeelekea kwenye uchaguzi wa Nigeria na mhariri ametazama zaidi kilichojitokeza siku ya kwanza ya uchaguzi huo na namna mitandao ya kijamii ilivyofurika habari kuhusu uchaguzi huo.
Mitandao ya kijamii ilifurika vidio zinazoonesha magenge ya vijana hasa katika mji wa Lagos wakivamia vituo vya kupiga kura ,na kuharibu vifaa vya upigaji kura,na kutumia nguvu kuwazuia wapiga kura waliopiga foleni kwa muda mrefu kuendelea na zoezi la kupiga kura. Mhariri huyo anasema haiwezekani kwamba nchi hiyo kubwa barani Afrika imeshindwa kuandaa uchaguzi wa kuaminika,huru na wa haki. Tume ya uchaguzi INEC haikuwa na mipango mizuri na ni jambo la kushangaza kwamba uchaguzi haukuakhirishwa. Hata hivyo mhariri anaongezea kwa kusema nchini Nigeria hili ni jambo la kawaida. Lakini kwa upande mwingine anauliza pamoja na yote hayo je mtu anaweza kusema uchaguzi huu umefanikiwa?
Anakumbusha kwamba ukilimulika eneo la Afrika Magharibi utagundua kwamba nchini Mali,Burkina Faso na Guinea hakuna tena tawala za zilizochaguliwa kwa njia za kidemokrasia. Na hilo pia ndilo linaloshuhudiwa katika nchi Tschad na Jamhuri ya Afrika ya Kati. Japo nchini Nigeria mara nyingi zinakuwepo fununu za kwamba jeshi linaweza kutwaa madaraka lakini hali halisi ni tafauti. Nchi hiyo hufanya mabadiliko kupitia sanduku la kupiga kura.
Rheinische Post
Gazeti la Rheinische Post Limezungumzia maonesho makubwa ya filamu barani Afrika ya Ougadougou-Burkifaso yaliyofunguliwa mwishoni mwa juma.
Mhariri anasema maonesho hayo yamekuwa yakiathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na kugubikwa na ugaidi na vurugu zinazotokea nchini Burkinafaso.
Kimsingi maonesho hayo makubwa ya filamu Afrika yanayojulikana kama FESPACO yalianzishwa mwaka 1969 na yamekuwa yakifanyika kila baada ya miaka miwili. Mhariri huyo anasema maonesho ya mwaka huu yamefanyika licha ya kuwepo kitisho cha ugaidi.