Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika
27 Oktoba 2023Die Zeit
Wiki hii lmeandika kuhusu safari inayotarajiwa hivi karibuni ya Rais wa shirikisho la Ujerumani, Frank Walter Steimeier nchini Tanzania. Kati ya mengi atakayoyafanya nchini humo ni kutembelea kwenye maeneo ambako wakoloni wa Kijerumani walifanya uhalifu. Steinmeir katika ziara yake hiyo ya siku tatu ataelekea katika mji wa Songea wenye takribani wakaazi 280,000. Mji huo ulipewa jina hilo ambalo lilikuwa la kiongozi wa enzi za vita vya Majimaji Songea Mbano. Wakati huo, mwaka 1905 wenyeji walipambana kupinga kutumikishwa kwa nguvu na utawala wa Kijerumani, kuporwa ardhi yao na kushurutishwa kuyahama makazi yao. Inakadiriwa kuwa watu wasiopungua 300,000 walipoteza uhai wao katika vita hivyo ambapo viongozi wa vita hivyo akiwemo Songea Mbano walinyongwa mbele ya familia zao:
Mhariri ameandika, waathiriwa wa dhuluma hizo zilizofanywa na utawala huo wa zamani wa kikoloni wa Ujerumani wanataka Rais Steinmeier ajumuike nao kuwakumbuka ndugu zao waliokuwa waathiriwa wa vita hivyo. Gazeti hilo limemnukuu Mwanahistoria na mmoja wa watafiti wakubwa wa historia raia wa Tanzania Nancy Rushohora akisema kuwa ni vizuri kuwa Steinmeier anafanya ziara hiyo lakini, ni lazima afike na majibu.
Neue Zürcher
Limeuzungumzia mgogoro wa Uhamiaji na safari hii ni kuhusu hatua ya Rais wa Tunisia Kais Saeid kukataa fedha za Umoja wa Ulaya zilizopangwa kusaidia nchi hiyo kulinda doria katika bahari ya Mediterania wakati kiwango cha wahamiaji wanaovuka bahari hiyo kuelekea Ulaya ikizidi kupaa. Gazeti hilo limeeleza kuwa, Rais Saed amekataa msaada huo wa fedha lakini bila uungwaji mkono kutoka mataifa ya kigeni, uchumi wa Tunisia uko hatarini. Zaidi limeandika kuwa, yeyote anayezungumzia uhamiaji Tunisia anazungumzia pia kuhusu fedha. Fedha kutoka Umoja wa Ulaya au Shirika la fedha la Kimataifa na kwamba zinaweza kusaidia hazina tupu ya Tunisia walau kwa muda mfupi.
Mwanzoni mwa mwezi Oktoba, Rais Kais Saed alikubali fedha kutoka Ulaya ambazo zilitolewa kama msaada wa kipindi baada ya janga la UVIKO. Lakini baada ya majibizano ya wazi katika mitandao ya kijamii kuhusu makubaliano ya uhamiaji yenye utata kati ya Waziri wa mambo ya kigeni wa Tunisia na Kamishna wa masuala ya uchumi wa Umoja wa Ulaya Oliva Varhelyi, Tunisia iliurejeshea umoja huo fedha zake kiasi cha Euro milioni 60. Makubaliano hayo ya uhamiaji kati ya Brussels na Tunisia yanalenga kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoingia Tunisia na kisha kuelekea mataifa ya Ulaya.
die tageszeitung
Gazeti hilo limeeleza namna mataifa ya Afrika yalivyogawanyika katika kuujadili mzozo wa Mashariki ya Kati. Limeandika kuwa, Kenya na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo zimeweka wazi kuwa upande wa Israeli wakati Afrika ya Kusini imetangaza kuwa iko Pamoja na Wapalestina.
Umoja wa nchi za Afrika umekuwa ukijipambanua kuwa usioegemea upande wowote katika mgogoro kati ya Israel na Hamas. Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Afrika, Moussa Faki Mahamat aada ya shambulio la Oktoba 7, alizitaka pande hizo mbili za mzozo kumaliza uhasama na kufanya mazungumzo bila masharti kuhusu suluhisho la kuwa na nchi mbili yaani Israel na Palestina.
Zaidi die tageszeitung limesema kwa upande wa Afrika ya Kusini, madai ya kufanyika kwa mawasiliano kati ya Waziri wa mambo ya kigeni Naledi Pandor na kiongozi wa kundi la Hamas Ismail Haniyeh kulisababisha mtafaruku. Inasemekana kuwa Pandor alifanya mazungumzo na Haniye na kuonesha kuiunga mkono operesheni ya kundi Hilo la Hamas. Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Afrika ya Kusini Clayson Monyela alitoa ufafanuzi kuwa katika mazungumzo hayo ya simu Waziri Pandor alionesha kusimama na watu wa Palestina na kuwaunga mkono, lakini pia alielezea kusikitishwa kwake na vifo vya watu wa Israel na Palestina wasio na hatia
Zeit Online
Limezungumzia kuhusu kuondoka kwa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA. Limeanza kwa kueleza kuwa, Umoja wa mataifa uliwaondoa wanajeshi wake katika kambi mbili ndani ya siku chache kabla ya muda uliopangwa, kutokana na kuhofia usalama wao. Mamia ya wanajeshi wa Ujerumani bado wapo nchini humo. Ni kutokana na hali mbaya ya usalama katika eneo la Kidal kaskazini mwa Mali.
Jumamosi iliyopita, vikosi vya kulinda amani waliondolewa katika kambi iliyo karibu na mji wa Tessalit. Taifa hilo la Afrika ya Magharibi limekuwa likikabiliwa na waasi wenye itikadi kali za kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo tangu mwaka 2012. Waasi hao waliendelea kusambaa baadaye katika nchi jirani za Niger na Burkina Faso.
Tangu mwaka 2013, wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wamekuwa wakishiriki kuhakikisha amani kwa raia na taifa hilo kwa ujumla. Zeit limearifu kuwa, tangu yalipotokea mapinduzi ya mwaka 2020, watawala wa kijeshi wa Mali, katikati mwa mwezi Juni, waliamuru Ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa uondolewe nchini humo. Awali watawala hao walishavitaka vikosi vya ufaransa viondoke pia, na sasa wanawategemea zaidi wapiganaji mamluki wa kundi la kampuni ya Wagner ya Urusi.