Magazeti ya Ujerumani kuhusu Afrika
17 Novemba 2023Frankfurter Allgemeine
Juma hili, mengi yameandikwa kuhusu uamuzi wa mahakama ya juu ya Uingereza wa kubatilisha mpango wa serikali wa kuwapeleka Rwanda wahamiaji wanaoingia nchini humo. Gazeti la Frankfurter Allgemeiner limeandika pia kuhusu uamuzi huo dhidi ya serikali ya Waziri Mkuu Rishi Sunak unaowahusu wahamiaji ambao ni wale wasiofuata taratibu za kisheria wanaoingia Uingereza kwa boti wakitafuta hifadhi.
Uamuzi huo uliotolewa Jumatano ulibainisha kuwa makubaliano ya kuwapeleka Rwanda waomba hifadhi hao ni batili kwa kuwa watakapofika nchini humo wanaweza kurejeshwa kwenye mataifa yao yanayokabiliwa na mizozo.
Frankfuter Allgemeine linakumbusha kuwa wakati wa utawala wa aliyekuwa Waziri mkuu Boris Johnson, Uingereza ilifanya makubaliano hayo ya kupeleka waomba hifadhi na taifa la Rwanda na kwa kufanya hivyo nchi hiyo ya Afrika ya Mashariki ingepokea misaada ya maendeleo kutoka Uingereza.
Linaandika kuwa tangu wakati huo London imedai kuwa uamuzi huo kimsingi ulikusudia kupunguza wimbi la wahamiaji wanaoingia Uingereza kinyume cha sheria kwa kutumia usafiri wa boti wakitokea Pwani ya Ufaransa.
die tageszeitung
Tuliangazie sasa die tageszeitung. Lenyewe limeandika kuhusu mafanikio lililoyapata Jeshi la Mali baada ya kufanikiwa kuukomboa mji wa Kidal. Eneo hilo lilikuwa likidhibitiwa na waasi wa Tuareg tangu mwaka 2014
Gazeti hilo linaeleza kuwa, baada ya muongo mmoja jeshi la Mali limetangaza hatua hiyo ya kushangaza ya kuukomboa mji wa Kidal wenye wakaazi wasiopungua 300,00. Japo mji huo ni mdogo ni wa kimkakati na umebeba alama kubwa na umekuwa ngome muhimu ya waasi wa Tuareg.
Serikali ya Mali haijawahi kuwa na udhibiti kamili wa eneo hilo baada ya uasi wa kabila la Tuareg wa mwaka 2011 na 2012. Mji huo uliangukia mikononi mwa waasi mwaka 2014 mara tu baada ya ziara ya Waziri Mkuu Moussa Mara, hali iliyosababisha mapambano kati ya jeshi na waasi hao.
die tageszeitung limefafanua zaidi kuwa, mapigano ya hivi karibuni ya kuukomboa mji wa Kidal, yalitangazwa wiki mbili zilizopita, wakati mashambulizi ya anga yalipowauwa watu 15 wakiwemo watoto. Mapambano hayo yalianza muda mfupi baada ya awamu ya mwisho ya jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa MINUSMA kuondoka Kidal ambapo baada ya kuondoka kwao waasi Wakituareg mara moja walizidhibiti kambi zao.
Gazeti hilo hilo, limeandika kuhusu mzozo wa Sudan. die tageszeitung limeanza kwa kichwa cha Habari kinachosomeka Vita vya Sudan: Mapambano ya kuwania madaraja ya mto Nile
Limeanza kueleza kuwa, baada ya awamu kadhaa za mazungumzo mapya yaliyofanyika mjini Jeddah bila ya makubaliano ya kusitisha vita kati ya makundi pinzani wiki iliyopita, mapigano katika mji mkuu wa Sudan, yameanza tena.
Jebel Aulia na bwawa lake katika mto Nile ni eneo la kimkakati kwa kuwa ni moja ya madaraja machache ambayo chini yake unakatiza mto huo mkubwa na kuigawanya Sudan katika pande mbili. Jumapili, wanamgambo wa RSF walianzisha mashambulizi wakililenga daraja la Jebel Aulia siku moja baada ya daraja la Shambat kuharibiwa mjini Khartoum. Daraja la Shambat linaunganisha sehemu ya kaskazini ya mji mkuu na mji Jirani wa Omdurman katika ukingo wa upande wa magharibi mwa mto Nile.
Kwa wanamgambo wa RSF mjini mjini Khartoum, daraja hili lilikuwa pia na umuhimu mkubwa. Hivi karibuni kiwanda muhimu zaidi cha kusafisha mafuta cha Sudan El Jeili kilicho takriban kilometa 70 kaskazini mwa mji huo mkuu, pamoja na majengo muhimu kama vile Wizara ya Mafuta na hospitali vimekuwa vikilengwa na mashambulizi.
Zeit Online
Gazeti la mtandaoni la Zeit limeandika kuhusu kuuwawa kwa watu wanaokadiriwa kufikia 70 katika shambulio lililofanywa na wanamgambo wenye itikadi kali kaskazini mwa Burkina Faso.
Zeit linaarifu kuwa, katika tukio hilo lililofanywa kwenye Kijiji cha Zaongo Novemba 5, waathiriwa wakubwa walikuwa wanawake na wazee. kama ilivyotangazwa na mwendesha mashtaka nchini humo Simon B Gnanou. Mbali na kuuwawa kwa raia, nyumba kadhaa zilichomwa moto.
Gazeti hilo limeinukuu taarifa kwa vyombo vya Habari kuhusu shambulio hilo ikieleza kuwa kwa uchunguzi uliofanyika hadi sasa na kauli za watu walioshuhudia mkasa huo, waliohusika na uhalifu huo bado hawajafahamika.
Kulingana na tafiti zilizofanywa na shirika linalohifadhi taarifa za maeneo yenye mizozo la ACLED, zaidi ya watu 7,000 wameshauwawa Burkina Faso kwa mwaka huu pekee. 1,700 kati ya hao wameuwawa kutokana na mapigano yaliyowalenga raia. Wanamgambo wenye itikadi kali nao wamekuwa wakitega mabomu au kuvishambulia vijiji.
Zeit linahitimisha kwa kusema, kwa miaka mingi Burkina Faso imekuwa ikipambana na wanamgambo wenye itikadi kali. Kwa upande wa mataifa Jirani, Mali na Niger, makundi ya kigaidi yamesambaa, baadhi ya hayo yana uhusiano na wanamgambo wa al Qaeda na kundi linalojiita dola ya Kiislamu, IS.