Magazetini: Kizungumkuti kumpata rais wa Kemisheni ya Ulaya
2 Julai 2019Viongozi wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya ambao wamekuwa wakikutana mjini Brussels tangu Jumapili, wameshindwa hadi sasa, kukubaliana juu ya mtu atakayerithi urais wa kamisheni ya Umoja wa Ulaya baada ya kuondoka rais wa sasa Jean Claude Juncker. Walitarajia kupata muafaka siku ya kwanza, lakini mazungumzo yaliendelea jana Jumatatu na kuambulia patupu kwa mara nyingine, na bado Jumanne wanaendelea kujaribu.
Matakwa ya wapigakura yanakiukwa
Gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung limeandika kuwa hukumu kuhusu mbio hizo ndefu za kutafuta mtu atakayechukua wadhifa wa juu zaidi katika Umoja wa Ulaya, sio ya kufurahisha. Mchakato wa kusaka muafaka unakiuka matakwa ya wapiga kura. Ni kawaida ya Umoja wa Ulaya kuyakusanya maslahi mengi katika kapu moja, na hilo mtu hawezi kulibeza.
Manfred Weber, ambaye muungano wake wa kisiasa umepata kura nyingi zaidi katika uchaguzi wa bunge la Ulaya, hana wingi wa viti vya kutosha kumuunga mkono. Na sasa, bunge na baraza wanamtaka Frans Timmermans ambaye muungano wake ulishika nafasi ya pili, wanayeamini anayo haiba zaidi, na hivyo kuweza kuwa angalau na hali ya kukubalika. Umoja wa Ulaya haupaswi kuwa katika mzozo wa kitaasisi.
Kuahirisha kuliepusha shari
Juu ya mada hiyo hiyo, gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger linasema hali ingeweza hata kuwa mbaya zaidi, kama viongozi wa nchi za Ulaya wangeendeleza mjadala katika kikao chao cha jana kilichoahirishwa. Linasema ilibidi mjadala huo wa Jumatatu usimamishwe, kwani vinginevyo mpasuko ungekuwa mkubwa zaidi, hasa kutokana na nchi kubwa za Poland na Italia ambazo zilihisi zimelaghaiwa. Hali hiyo ingedhoofisha ushirikiano katika Umoja wa Ulaya ambao tayari sio wa kuridhisha. Kuahirisha mkutano huo kumewapa wadau fursa ya kujipanga, na hilo sio geni katika Umoja wa Ulaya, ambapo kila kitu kina gharama yake, hata kumchagua kiongozi.
Ushujaa wa Bi Rackete
Gazeti la Rhein-Zeitung la mjini Koblenz limemzungumzia Bi Carola Rackete, nahodha wa meli ya uokozi iitwayo Sea Watch 3, ambaye anakabiliwa na kesi nchini Italia, baada ya kuwanusuru wahamiaji baharini, na kutia nanga katika bandari ya Lampedusa nchini Italia bila ruhusa.
Linasema Rackete ambaye ni raia wa Ujerumani nai kinyume na Matteo Salvini, waziri wa mambo ya ndani wa Italia aliye hasimu kwa wahamiaji. Linasema dhamira yake haikuruhusu kuwaacha binadamu wazame baharini, licha ya kujua hatari inayomsubiri kutoka kwa wanasiasa wa sera kali za mkono wa kulia, na linasema kwa kitendo chake hicho, Carola Rackete ni shujaa wa nyakati hizi.
dpae