Magazetini leo
23 Julai 2012Tukianza na gazeti la Volksstimme la mjini Magdeburg, linazungumzia kuhusu tamko la chama cha SPD kuhusu ilani ya chama hicho katika uchaguzi mkuu. Gazeti linaandika kuwa ni jambo la kushangaza: Chama cha SPD hivi karibuni kimeunga mkono kuipatia sekta ya mabenki nchini Uhispania mabilioni ya euro, na sasa kiongozi wa chama hicho, Sigmar Gabriel, anajaribu kuyashutumu mabenki. Ikihitajika chama hicho kitasaidia kutoa fedha nyingine za msaada. Kitu ambacho chama hicho kinajaribu kufanya hapa ni kuyumba kisiasa. Ndio sababu tamko hilo la ilani ya uchaguzi linalenga zaidi katika kupunguza nguvu za mabenki. Bila shaka, inaonesha serikali ya muungano inaweza kupambana kwa nguvu dhidi ya tamko hilo. Iwapo pande hizo mbili katika kampeni za uchaguzi mwishoni mwa mwaka ujao zitavutana kuhusu mada hii ya kuvutia , wapiga kura hawatapenda kamwe kuvileta pamoja vyama hivyo katika kuunda tena serikali ya mseto.
Kuhusu mada hiyo gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung linaandika.
"Haishangazi kuwa mkakati wa chama cha SPD katika uchaguzi mkuu umeanza kuingiwa na hali ya wasi wasi. Mkakati wa mapambano hauna tena mafanikio? Linauliza gazeti hilo."
"Rais wa Ufaransa, Francois Hollande, ameonyesha jinsi mambo yanavyopaswa kufanyika. Chama cha SPD kimeamua kupigana vita hii kwa mitindo ya kizamani. Kile kilichobaki sasa ni kushambulia kila mtu ambaye anaonekana kuwa ni chanzo cha uovu. Kwa hapa ni viongozi wa mabenki na wale ambao wanafaidika na mzozo wa kifedha. Sigmar Gabriel, kiongozi wa SPD, mwishoni mwa juma katika ukosoaji wake wa mabenki ameanza kuyapima maji."
Kuhusu mada ya kashfa ya wagonjwa wanaosubiri kupatiwa viungo vya mwili, gazeti la Badische Neueste Nachrichten linaandika.
"Kwa nguvu kabisa wanasiasa na chama cha madaktari wamejaribu kuzungumzia kuhusu kashfa ya kupatikana viungo vya mwili ambavyo wangonjwa wanasubiri kupatiwa. Mambo mengi yanaonekana katika mchezo huu. Data za wagonjwa wanaosubiri kupatiwa matibabu zimefanyiwa udanganyifu ili kuweza kupata viungo vingi zaidi na kufanya biashara haramu, na hii pia inahusu kuwalazimisha wagonjwa ambao wako katika hali mbaya kuweza kutoa baadhi ya viungo vyao. Huu ni uhalifu ambao uko katika mtindo wa kundi la mafia la kihalifu."
Gazeti la Neue Presse, likiandika kuhusu mada hiyo, linasema.
"Ni udanganyifu mkubwa kabisa ambao una matokeo mabaya. Watu 12,000 wanahitaji kwa haraka viungo ili waweze kuishi tena. Taarifa hii inalifanya tatizo hilo kuwa kubwa zaidi. Lakini hivi sasa kuna ushahidi unaolekeza kuwapo na uhalifu, na iko haja ya kuchukuliwa hatua kali madaktari watakaobainika kuhusika, na pia kunapaswa kuwa na udhibiti wa kutosha wa chombo kinachohusika na masuala hayo."
Na mwisho ni kuhusu mjadala juu ya uamuzi wa mahakama kuzuwia wanaume kufanyiwa tohara, hasa watoto, kwa misingi ya kidini. Gazeti la General Anzeiger la mjini Bonn limeandika.
"Kuna katiba inayozungumzia haki za binadamu ambayo hapa inagongana. Hakuna dini nchini Ujerumani ambayo iko juu ya katiba. Swali ni kiasi gani ambacho katiba hiyo inaweka mipaka na inaweza pia kuruhusu. Ingefaa kungefanyika mjadala huru ambao hautawashirikisha viongozi wa dini wa pande zote."
Gazeti la Sächsische Zeitung kutoka mjini Dresden likiandika kuhusu mada hiyo linasema.
"Mada hii tete inapaswa kupatiwa maelezo. Na ni sahihi mwishowe kuwa hakuna sheria , kwamba tohara zinazofanywa kwa misingi ya kidini zizuiliwe, hata baada ya kuwapo uchunguzi wa maoni ya watu unaopendelea sheria hiyo. Upigaji marufuku utakuwa jambo la kipekee, ambalo Ujerumani inapaswa kujiepusha nalo."
Mwandishi : Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Othman Miraji