Magazetini: Marekani yahamishia ubalozi wake Jerusalem
15 Mei 2018
Gazeti la Neue Osnabrueker Zeitung likiandika kuhusu mzozo wa mashariki ya kati, linasema:
"Kuutambua mji wa Jerusalem kama mji mkuu wa Israel kunaweza kuzungumziwa tu kama vile mchezo wa karata, wakati rais Donald Trump akisubiriwa kuja na mpango mahsusi wa amani, ambao unaweza kuwaleta karibu Wapalestina na Waisrael katika suluhisho la mataifa mawili. Iwapo Israel itakuwa tayari kuonesha maridhiano na Palestina baada ya zawadi ya kidiplomasia kutoka Marekani, kwa mfano katika sera zake za kujenga makaazi ya Wayahudi, hilo lina shaka. Uamuzi wa Trump kuhusu Jerusalem na kujitoa katika mkataba wa kinyuklia na Iran inaweza kuwa ishara mbaya. Moto unawaka katika mashariki ya kati. Kufikiria kwamba Umoja wa Ulaya unaweza kujitoa, si jambo linalotarajiwa. Mbaya zaidi , hakuna mtu ambaye anaweza."
Mhariri wa gazaeti la Badische Zeitung la mjini Freiburg akizungumzia kuhusu kuhamishwa kwa ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Jerusalem, anasema kwamba wakati Waisrael wanashangilia kufunguliwa kwa ubalozi huo, Ukanda wa Gaza kunawaka moto. Mhariri anaendelea kwa kusema:
"Ni mara chache maandamano yamekuwa makubwa na ya hasira kama yalivyo sasa, wakati Marekani inafanya juhudi za kuzipatanisha Israel na Palestina. Haya ni matokeo ya uamuzi wa Trump. Kila mmoja anafahamu, kwamba gharama iko juu mno. Na nani analazimika kulipa ?"
Miaka 70 ni historia ya mafanikio, anasema mhariri wa gazeti la Pforzheimer Zeitung anapozungumzia Israel kutimiza miaka 70 tangu kuundwa taifa hilo. Mhariri anasema:
"Waisrael wamelifanya jangwa kuweza kutumika tena kama sehemu ya kilimo, wamefanikiwa kutatua matatizo yao ya maji kwa teknolojia ya kisasa ya kuchuja maji ya chunvi na ni viongozi duniani wa maeneo mengi katika teknolojia ya kompyuta. Mamilioni ya wahamiaji wamejumuishwa katika jamii ya Kiyahudi. Lakini kuanzia jana baada ya kusherehekea kuundwa kwa taifa hilo kuna picha nyingine ya kumbukumbu. Dazeni kadha za Wapalestina wameuwawa na idadi kubwa ya wengine wamejeruhiwa, wanajeshi wa Israel wenye silaha, matairi yanayochomwa moto, na wingu la mabomu ya kutoa machozi."
Nalo gazeti la Stuttgarter Nachrichten linazungumzia kuhusu wachezaji wawili wa timu ya taifa ya Ujerumani Mesut Ozil na Ilkay Gundogan waliokutana na rais wa Uturuki Tayyip Erdogan. Mhariri anaandika kwamba ingekuwa bora zaidi kandanda likatenganishwa na masuala ya kisiasa:
Mhariri anaandika:
"Katika hali hii Mesut Ozil na Ilkay Gundogan wamefanya kinyume chake, na hii ni ishara mbaya kabisa. Iwapo wamefanya hivi kutokana na ujinga , ama walifanya hivi kwa kujitambua na makusudi kabisa, hilo halina umuhimu hapa. Ukweli ni kwamba hawakuvuruga tu ushindani kati ya chama cha soka cha Ujerumani kuwania kuwa mwenyeji wa fainali za kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2024 , dhidi ya Uturuki , lakini pia nchi yao, ambayo kwa miaka kadhaa wachezaji hao wamefanikiwa kucheza kandanda na pia Ujerumani kumzuwia Erdogan kutokana na sababu muhimu kufanya kampeni ya uchaguzi wa rais hapo Juni 24 nchini Ujerumani. Ozil na Gundogan hadi sasa ni mfano mzuri wa ujumuisho katika timu ya taifa ya Ujerumani. Kutokana hayo waliyofanya, mtu anaweza kujiuliza iwapo wachezaji hao wanastahili kuwamo katika kikosi cha timu ya taifa kinachokwenda katika fainali za kombe la dunia?"
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga