1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Mgogoro wa fedha wa nchini Uturuki

16 Agosti 2018

Yaliyoandikwa katika tahariri za magazeti ya Ujerumani ni pamoja na mgogoro wa fedha nchini Uturuki ambako,maafa yaliyotokea nchini Italia baada ya daraja moja kuvunjika.

Türkei,  Gumushane:  Recep Tayyip Erdogan hält eine Rede
Picha: picture-alliance/AA/M. Kaynak

Stuttgarter Nachrichten 

Mhariri wa gazeti hilo anasema jambo la kuzingatia hapa ni jinsi mustakabal wa Uturuki utakavyokuwa katika ngazi ya kimataifa. Lakini kwa sasa inaonekana kana kwamba Rais Recep Erdogan anaelekea zaidi katika upande wa China na Urusi kuliko Ulaya ama Marekani. Msimamo huo ni wa kushangaza kiuchumi. Nchi ya Uturuki ambayo ni mwanachama wa NATO katika upande wa mashariki imekuwa mshirika anayeyumbayumba. Mara inashaka na huyu na mara na yule. Mkakati huo hautafua dafu kwa kipindi kirefu ndani na nje ya nchi ya Uturuki.

Mannheimer Morgen

Gazeti la Mannheimer Morgen linayazungumzia maafa yaliyoteka nchini Italia baada ya daraja lililoporomoka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 35. Lakini mhariri wa gazeti hilo anayazungumzia maafa hayo kwa kupima hisia za watu nchini Ujerumani na anasema, muda mfupi tu baada ya daraja hilo kuanguka Ujerumani imepatwa na taharuki.Watu wanauliza jee madaraja yetu yako salama kwa kiasi gani? Jee bado inawezekana kwa mtu kuvuka madaraja na mito bila ya kuwa na wasiwasi. Jibu ni kwamba zipo habari nzuri na mbaya. Kwanza ndio, inawezekana kuvuka kwenye madaraja na mito bila ya wasiwasi. Sababu ni kwamba sera thabiti ya idara husika ambayo mara nyingine inakosolewa, ya kuhakikisha usalama wakati unaostahili, inahakikisha kwamba madaraja yenye mashaka hayatumiwi na wananchi lakini habari mbaya ni kwamba fedha kwa ajili ya kuwekeza katika miundo mbinu haziongezeki.

Daraja lililovunjika nchini ItaliaPicha: Imago/Xinhua/A. Lingria

Allgemeine Zeitung

Mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung anatoa maoni juu ya uamuzi wa mahakama ya hapa nchini Ujerumani wa kutambua rasmi jinsia ya tatu, licha ya zile za jadi za mwanamke na mwanamume. Lakini mhariri huyo anataka ufafanuzi juu ya dhana hiyo kutoka kwa waziri wa masuala ya jamii Franziska Giffey aliyesema kwamba jinsia mbalimbali zinapaswa kutambuliwa na kuimarishwa. Mhariri huyo anaeleza kwamba ni jambo la kukasirisha kusikia waziri huyo akizungumzia juu ya kuwepo jinsia mbalimbali. Jee anachomaanisha ni nini hasa anaposema jinsia mbalimbali? Lakini jambo la kushangaza zaidi ni mtazamo wa chama cha kijani na ule wa watetezi wa watu waliobadilisha jinsia, msimamo wa kupinga watu hao wa jinsia ya tatu wathibitishwe na madaktari. Yafaa kukumbuka kwamba katika hali nyingi uthibitisho wa daktari ni wa lazima.

Neue Westfälische

Mhariri wa gazeti hilo ametoa maoni juu ya mkasa wa mtu anayetuhumiwa kwamba alikuwa mpambe wa aliekuwa kiongozi wa mtandao wa kigaidi wa Al-Qaida, Osama bin Laden. Mtu huyo anayefahamika kwa jina la Sami A. aliondolewa kwa nguvu nchini Ujerumani na kupelekwa Tunisia kwa madai kwamba yeye ni mtu hatari mweye itikadi kali za kiislamu.Hakimu mmoja sasa anazilaumu idara za Ujerumani kwa kuchukua hatua hiyo.

Mhariri wa gazeti la Neue Westfälische anatoa maoni yake juu ya mkasa huo kwa kutolea mfano pale mahakama inapo muondolea mtu tuhuma za kufanya shambulio la bomu lakini polisi inaendela kuzishikilia tuhuma hizo. Mhariri huyo anasema huko ni kuvunja sheria na katiba ya nchi. Hilo halikubaliki. Hakika lingekuwa jambo sahihi kuchunguza tuhuma za ugaidi zinazomkabili mtu ili kuweza kumchukulia hatua ya kumfukuza nchini au kumpekela jela kwa miaka mingi baada ya kuthibitisha makosa yake.

Lakini kuchukua hatua kinyume na hukumu iliyotolewa na mahakama ni kukiuka taratibu za nchi yenye utawala wa kisheria. Na anayefanya hivyo anawanufaisha maadui wa utawala wa kisheria yaani makundi ya watu wenye itikadi kali za mrengo wa kulia ambao ni maadui wa katiba.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

  

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW