1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini: Mjadala wa vyama vidogo vya kisiasa wafanyika

5 Septemba 2017

Katika maoni ya magazeti ya Ujerumani leo hii wahariri wengi wanatoa maoni juu ya mjadala wa televisheni ambapo viongozi wa vyama vidogo vya kisiasa walishiriki katika mjadala kabla ya uchaguzi wa Ujerumani wa tarehe 24.

Deutschland - Live-Fünfkampf der kleinen Parteien in der ARD
Picha: picture-alliance/B. v. Jutrczenka

Tunaanza na maoni ya gazeti la Mittelbayerische Zeitung ambapo mhariri anazungumzia juu ya kile kinachoitwa pambano la vyama vidogo. Anasema vyama hivyo vinazidi kuwa muhimu kwa sababu vinaweza kuwa na dhima kubwa katika mchakato wa kuunda serikali ya mseto mhariri wa gazeti hilo ameandika. Ushindani mkubwa kutoka kwa wapinzani wa kisiasa haukuwepo, licha ya kwamba watu wapatao milioni 16 waliutazama mjadala huo kwenye televisheni zao. Mhariri anasema kutokana na mjadala uliotangulia wa viongozi wa vyama vikuu vya kisiasa hakuna dalili kuwa kampeni  moto moto za  uchaguzi zitafanyika. Katika mwaka huu vyama vidogo ndio vitatoa cheche lakini cheche hizo zitakoleza moto katika sehemu ndogo tu kwani juhudi wanazozifanya kwa sasa katika kampeni za uchaguzi wa mwaka 2017 zimechelewa.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Rundschau ameandika juu ya mkutano wa kilele uliofanyika Berlin hapo jana kujadili hatua za kukabiliana na athari katika mazingira zilizosababishwa na magari yanayotumia dizeli na ameandika. Serikali kuu imeahidi kuongeza Euro milioni 500 kwenye mfuko utakaotumiwa kwa ajili ya kutekeleza hatua za kuzikabili athari hizo.Swali ni Je, kwa nini zisitolewe fedha nyingi zaidi kwa ajili ya kuendeleza usafirishaji utakaozingatia usafi wa mazingira?  Kiasi cha Euro milioni 500 zilizotolewa na serikali kuu ili kuzikabili athari za hewa chafu hazitoshelezi sababu ni kwamba mchango utakaotolewa na viwanda vya magari utaendelea kuwa Euro milioni 250 tu. Inapaswa kutilia maanani kwamba viwanda vya kutengeneza magari ndivyo hasa vinavyofanya uchafuzi wa mazingira.

Kuhusu Korea Kaskazini na mpango wake wa kufanya majaribio ya makombora ya nyuklia  mhariri wa gazeti la Frankfurter  Allgemeine anaeleza maoni yake kwa kusema lingekuwa jambo jema zaidi endapo baadhi ya serikali zingepunguza kelele na badala yake zingejaribu kutayarisha dhana juu ya kulitatua tatizo la Korea ya Kaskazini kwa sababu kadiri vitisho vinavyozidi kutolewa na kusababisha hali ya wasiwasi ndivyo njia za kuutatua mgogoro huo zinavyopungua.

Gazeti la Nürnberger Zeitung linaitaka dunia iwe makini na kiongozi wa Korea ya Kaskazini na mhariri wa gazeti hilo anafafanua kuwa haitafaa kwa mtu yeyote kutaraji kwamba Kim Jong Un ataacha kufanya uchokozi na kuendelea kufanya majaribio ya silaha za nyuklia kinyume na baadhi ya watu wanavyofikiria.  Kiongozi huyo wa Korea Kaskazini si mwendawazimu. Kim Jong Un amejifunza jambo moja vizuri sana! Kwamba asiyemiliki silaha za nyuklia na endapo ataingia kwenye mvutano na Marekani basi atakuwamo katika hatari ya kushambuliwa.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW