Magazetini: Mkutano wa NATO, Trump aishambulia Ujerumani
12 Julai 2018Mhariri wa gazeti la Rheinpfalz la mjini Ludwigshafen anazungumzia kuhusu mkutano wa NATO na ukosoaji wa rais wa Marekani Donald Trump kwa Ujerumani.
Mhariri anaaandika kwamba Muuzaji ambaye anagombana na wanunuzi wake anaharibu kazi yake. Bila shaka rais wa Marekani Donald Trump ndivyo anavyofanya. Kwa anataka Marekani iuze gesi nyingi zaidi asilia kwa bara la Ulaya, anaishambulia Ujerumani kutokana na kuagiza gesi nyingi na hali hiyo anaiita kuwa "mfungwa wa Urusi. Kwa hiyo sio tu mzozo wa kibiashara wa Trump, lakini pia matamshi yake ya kijinga yanaharibu muonekano wa Marekani. Kuishutumu Ujerumani kwamba inaifanya Urusi kuwa tajiri na pia kwamba Ujerumani itakuwa inaitegemea zaidi Urusi ni jambo lisilo na msingi. Kwa miongo kadhaa mataifa ya Ulaya yamekuwa yakitegemea gesi kutoka katika eneo la Siberia. Kama mshiriam wa kibiashara Urusi wakati huo ilikuwa yenye kuaminika kuliko ilivyokuwa Marekani. Madai ya Trump sio ya kweli kama zilivyo hesabu zake. Ujerumani haipati mahitaji yake ya nishati kwa asilimia 70 kutoka Urusi, lakini chini ya asilimia 40 tu.
Nae mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung akizungumzia mkutano wa kilele wa NATO anasema, sentensi muhimu kuhusiana na siasa za Marekani chini ya Trump aliisema Merkel zaidi ya mwaka mmoja uliopita katika hema la bia mjini Munich katika eneo la tamasha la bia kule Trudering. Wakati huo Merkel alisema, muda ambapo tumezowea kubweteka, umepita. Watu wa Ulaya tunapaswa kuelekeza mustakabali wetu wenyewe. Matamshi haya ndio kwanza tunayabaini. Mataifa ya Ulaya, hususan Ufaransa na Ujerumani, yanapaswa kujitafakari , kwamba anaweza kuondoa mwanvuli unaotulinda na silaha za kinyuklia. Na baada ya hapo? Huenda kikosi cha kupambana na silaha za kinyuklia cha Ufaransa kilichopo Ulaya ya kati kikalazimika kuingilia kati. Kwa hali halisi ya hivi sasa huenda isiwe hivyo. Huenda matumizi ya asilimia 2 ya pato jumla la taifa haitakuwa kiwango cha mwisho. Tunaweza kufikia haraka lengo hilo la asilimia 2, kuliko tunavyopenda, iwapo Trump atavuruga uchumi wa dunia kupitia vita vya kibiashara. Asilimia 2 inaweza kufikiwa bila ya kuchukua hatua zaidi, kwa kuwa inawezekana kutokana na kunywea kwa uchumi.
Kuhusu hukumu dhidi ya Beate Zschaepe mwanamke anayedaiwa kuhusika na kundi la kigaidi, gazeti la Weser-Kurier la mjini Bremen, linaandika kwamba, wakili wa Zschaepe tayari alishasema, kwamba atakata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama hiyo. Wakili anadai kwamba mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 43 hakuwahi kabisa kuhusika katika tukio la shambulizi, kutambua kuwa hajawahi kuhusika kabisa na watu waliofanya mashambulizi. Hali hiyo inaweza kuleta msisimko mkubwa, kwasababu kundi hilo la washambuliaji linafahamika kwa kiwango kikubwa walikuwa wakifanya shughuli zao kwa karibu sana.
Naye mhariri wa gazeti la Allgemeine Zeitung la mjini Mainz akizungumzia kuhusu hukumu dhidi ya idara ya NSU linasema historia ya NSU ni historia ya kushindwa vibaya katika jamhuri ya Ujerumani. Kwa miaka mingi kumekuwa na wasi wasi wa kundi la mauaji na lilionekana kuwa halihusiki na mauaji hayo. Na kundi lililokuwa likiwasaidia lilitathminiwa kuwa na kiasi ya watu 100 hadi 200. Wengi wao bado hawajulikani ama hawajatiwa hatiani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse / deutschland
Mhariri: Mohammed Khelef