Magazetini: Trump na Putin wawindana Syria
12 Aprili 2018Tukianza na gazeti la Der tagesspiegel la mjini Berlin linaandika kuhusu mvutano unaoelekea katika mashambulizi ya muungano unaoongozwa na Marekani dhidi ya vituo vinavyotengeneza gesi ya sumu nchini Syria. Mhariri anaandika kwamba Trump anamtwika dhamana dikteta wa Syria Bashar al-Assad kwa shambulio la gesi ya sumu katika eneo lililokuwa linadhibitiwa na waasi la Douma. Mhariri anaendelea:
Syria pamoja na Urusi inayoitetea nchi hiyo zote zinapinga madai hayo, zikisema ni suala lililopangwa. Israel imekuwa ikifuatilia maeneo ambayo majeshi ya Iran yapo na Iran imetangaza kulipiza kisasi iwapo yatashambuliwa. Raia wa mataifa ya magharibi wanapaswa kudai kuwapo uwazi wa kutosha kutoka katika serikali zao kuhusiana na suala hili. Ushahidi kuhusiana na ufahamu wa mashirika ya kijasusi kuhusu tukio hilo hadi sasa haupo. Kuna sababu nzuri , Putin kama mtu hatari pamoja na Trump kuwazuwia , na kuyaamini mashirika ya kutetea haki za binadamu, badala ya kuunga mkono Israel katika mapambano dhidi ya utawala wa Assad na viongozi wa kidini wa Iran.
Nae mhariri wa gazeti la Westfälische Nachrichten la mjini Münster kuhusiana na mada hiyo anaandika, kwamba aina hii ya matamshi ya kivita yanakwenda mbali sana , kuliko ilivyokuwa hapo awali. Mhariri anaandika:
Hali ni mbaya kuliko ilivyokuwa. Trump anataka kulipiza kisasi, Putin anapinga. Ni vita vya maneno baina ya mataifa mawili yenye nguvu. Mpaka wa kuwa na burasa na majadiliano kwa pande zote mbili, umevukwa.
Wengi miongoni mwa watumiaji bilioni mbili wa mtandao wa kijamii wa facebook wenyewe wanamakosa. Anaandika mhariri wa gazeti la Der neue Tag la mjini Weiden kuhusiana na hatua ya kamati ya baraza la seneti nchini Marekani kumuita kwa mahojiano mkuu wa mtandao huo Mark Zuckerberg. Mhariri anaadika.
Wachache wanatambua kile walichokiweka na kukiacha katika mtandao huo. Kwasababu wengi hawaangalii matumizi yao ya msingi ya mtandao wa Facebook, ili kuzuwia ukusanyaji wa data unaofanywa na mtandao huo, ingekuwa somo kubwa kwa shirika hilo linalojitangaza kwamba lina nia njema na watumiaji wake kutoka Menlo Park. Na nani anajua , huenda mtandao huo wa kijamii ukapotea haraka kama ulivyojitokeza. Halafu kutajitokeza kitu kingine kikubwa katika ulimwengu wa digitali.
Mhariri wa gazeti la General-Anzeiger la mjini Bonn anazungumzia kuhusu mkutano wa kufahamiana miongoni mwa mawaziri wanaounda serikali ya mseto inayoongozwa na kansela Angela Merkel wa Ujerumani. Mhariri anaandika:
Nia ya kutaka kupata msimamo wa pamoja ilikuwapo, hali ya msisimko ilikuwa nzuri, alisema kansela Angela Merkel na makamu wake Olaf Scholz. Lakini haitoshi , haitoshi kabisa. Anaandika mhariri, kwa sababu hilo ni jambo la kawaida kwa serikali yenye uchumi mkubwa kabisa barani Ulaya, ili kulinda heshima ya kisiasa na kiuchumi ya nchi hii muhimu barani Ulaya. Serikali ambayo inatakiwa kuamua ina msimamo gani katika mzozo wa Syria, na jinsi gani itashughulikia vita vya kibiashara duniani. Na haitoshi, wakati waziri wa fedha Scholz akisema, kwamba kila kitu kitawezekana tu kwa kuwa na sera imara za bajeti. Hii ni kweli takriban iwapo hazina imejaa, uchumi unakua kwa kasi na uongozi unafanya vizuri.
Mwandishi: Sekione Kitojo / inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga