Magazetini: Uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki
21 Agosti 2018Tukianza na gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung la mjini Heidrlberg kuhusu uhusiano kati ya Uturuki na Ujerumani, mhariri anaandika kwamba rais wa Uturuki Erdogan kwa muda wa miaka miwili ameweza sio tu kuondoa utawala wa kisheria nchini mwake, bali pia ameharibu uchumi wa nchi hiyo. Mhariri anaendelea:
"Uchumi uliokuwa unakua kwa kasi umefikia mwisho. Kile pekee ambacho kinaendelea kuongezeka nchini Uturuki ni kodi. Katika hali hii kile ambacho dikteta huyo anachotaka ni msaada wa fedha kutoka Ujerumani. Ndivyo anavyotaka pia kiongozi wa chama cha SPD Andrea Nahles. Na ndio sababu huenda Erdogan anataka kumwachilia huru mmoja kati ya mateka wake wengi. Mwandishi habari Mjerumani Mesale Tolu, ambaye amefunguliwa mashitaka ya bandia kwamba ni msaliti."
Gazeti la Stuttgarter Nachrichten linazungumzia pia uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki kwa kuandika kwamba uhusiano huo ambao ni mbaya umeendelea kuwa mbaya zaidi. Na ndio sababu unajitokeza wazi mwelekeo wake, vile Ujerumani inavyotaka. Mhariri anaadika:
"Na kuna mwelekeo mmoja tu. Uturuki inabakia kuwa mshirika wetu muhimu kutokana na uhusiano mkubwa wa kijamii pamoja na maslahi ya pamoja ya kiusalama. Hii haina maana kwamba tunapaswa kuacha kila aina ya uwezekano wa uchokozi ama kupuuzia kila kashfa, ambayo uongozi wa Uturuki unajaribu kila wakati kuendesha mtandao wa ushawishi wa matukio ya kihalifu nchini Ujerumani. Lakini kwa kuwa kumekuwa na uhusiano wa karibu ambao ni karibu na kuwa katika familia moja, ni lazima tumuangalia ndugu katika hali nzuri na mbaya . Kwa hiyo majadiliano ni muhimu kuendelea."
Katika suala la kuachiliwa huru Mesale Tolu mwandishi habari wa Ujerumani nchini Uturuki , mhariri wa gazeti la Südwest Presse la mjini Ulm anaandika:
"Erdogan kwa hivi sasa anaihitaji Ulaya. Mchezo wake wa kujitoa muhanga dhidi ya Marekani unaipeleka nchi yake katika mzozo hatari. Bila ya uwekezaji, fedha za kodi na mikopo kutoka Ulaya zinatishia mtikisiko katika sarafu ya nchi hiyo kutumbukia katika hali ambayo haitaweza kudhibitika. Na hali hii haina maslahi kwa Uturuki ama Umoja wa Ulaya. Uturuki chini ya rais Erdogan inabaki kuwa mshirika asiyetabirika. Anatumia wafungwa wa kisiasa katika masuala ya siasa na kufunganisha na masuala ya sheria. Mambo yote hayo anayatumia kama nyenzo zake."
Kuhusu mada ya mwisho Ugiriki kupatiwa msaada zaidi, licha ya awamu ya mwisho ya msaada ukikaribia kumalizika. Mhariri wa gazeti la Volksstimme la mjini Magdenburg akizungumzia kuhusu suala hilo anaandika:
"Licha ya kiasi kikubwa cha mkopo na hatua madhubuti za kurejesha mkopo huo, bado Ugiriki imo katika matatizo. Kwa nini nchi hiyo inataka kufutiwa deni lake ifikapo mwaka 2032. Na vipi nchi hiyo inataka katika muda wa miaka 40 kutowajibika kuhusu masuala ya riba na ziada katika bajeti yake?. Kwa hivi sasa kila mmoja anamatumaini tu kwamba soko la fedha linaendelea kuwa na imani na sarafu ya euro, na kutoiacha Ugiriki kuporomoja."
Hayo ndio aliyoweza kutukusanyia Sekione Kitojo kutoka kwa baadhi ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman