Magazetini: Ziara ya Macron Marekani
26 Aprili 2018
Tukianza na gazeti la Badische Zeitung la mjini Freiburg kuhusu ziara ya Macron nchini Marekani, mhariri wake anaandika:
"Emmanuel Macron amekabiliana na karibu kila kitu ambacho kiongozi anachoweza kukabiliana nacho katika ziara ya kitaifa alipokutana na Donald Trump. Kushikana mikono kwa nguvu, mkono katika bega kila wakati, busu nyingi ambazo mtu hajawahi kuziona katika Ikulu ya Marekani ya White House. Macron anaingia katika hatari kubwa anasema mhariri. Wakati Macron anayefuata sera za kimataifa na Trump anayefuata zera za kizalendo zaidi wakijiweka pamoja, akitaka, mbali ya kwamba wanatofautiana kuhusiana na mkataba wa Iran, lakini anataka kujenga uhusiano imara na Trump. Ni katika mtazamo huu tu ambapo kila uhusiano wa kisiasa ni suala ambalo linaweza kufanyiwa majadiliano iwapo kuna maslahi. Macron, mhariri anaadika anaweza hatimaye kuondoka mikono mitupu."
Kuhusu ziara hiyo ya Macron nchini Marekani, mhariri wa gazeti la Mannheimer Morgen anasema baada ya ziara hiyo iliyokuwa na mapenzi makubwa ya Emmanuel Macron mjini Washington, Donald Trump anatarajia kukutana na Angela Merkel kesho katika ziara ambayo ni tofauti kabisa na yenye majadiliano magumu. Mhariri anaadika:
"Majukumu yanaonekana kuwa yamsingi kabisa. Rais wa Ufaransa alitayarisha uwanja kwa hisia, kansela wa Ujerumani yeye atakuwa anajadili kwa njia ya ukakamavu zaidi. Timu ya Ulaya ya M na M, Macron na Merkel inalenga katika lengo moja. Linahusu kuokoa makubaliano ya kinyuklia na Iran pamoja na kuzuwia ongezeko la ushuru wa forodha kwa bidhaa za chuma na bati kutoka katika mataifa ya Umoja wa Ulaya."
Chuki dhidi ya wayahudi
Tunavaa Kippa. Anaandika mhariri wa gazeti la Rhein-Neckar-Zeitung la mjini Heidelberg kuhusiana na vikofia wanavyovaa Wayahudi kuhusiana na mada ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani. Mhariri anaandika:
"Tulipaswa kuonesha wazi kwamba tunavaa vikofia hivyo na huenda ilitakiwa kufanya hivyo mapema zaidi, ili kuzuwia hali ya kutoeleweka. Kwamba Ujerumani inaikosoa Israel , kama yalivyo mataifa mengine, ni sahihi na ni haki kabisa. Lakini ukosoaji huo hata hivyo si suala la kuikana kabisa Israel, badala yake ni katika hali hiyo tu, ambayo ni katika kutofautiana kimawazo. Tunavaa Kippa, tunavaa hijabu. Na kwa kiasi kikubwa tunavaa misalaba. Haya yote yanapatikana nchini Ujerumani. Kwa hakika ni ujumbe wa wazi wa kuvumiliana."
Nae mhariri wa gazeti la Hannoversche Allgemeine Zeitung akizungumzia mada hiyo anaandika:
"Mshikamano dhidi ya chuki kwa Wayahudi ni ujumbe muhimu kwa sasa. Mjadala kuhusu chuki dhidi ya Wayahudi katika nyimbo za kurap nchini Ujerumani, vidio za kushitua za mashambulizi dhidi ya kijana wa Kiisraeli aliyevaa kibandiko mjini Berlin, maadhimisho ya miaka 70 ya kuundwa kwa taifa la Israel, haya yote yalikuja kwa pamoja wiki iliyopita na ilikuwa ni ajenda ya kisiasa. Lakini kama kawaida, pamoja na hayo yote, kuna kitisho cha kuporomoka kwa ishara ya mshikamano, na kupotea kwa maadili. Mtu hapambani dhidi ya chuki dhidi ya Wayahudi jioni. Na hii sio katika fikira za wanazi mamboleo ama Waislamu wenye itikadi kali pekee, lakini hata katika hukumu na kupunguza nadharia ambazo hazijafanyiwa uchunguzi."
Kuhusu mada ya mwisho ya rais mpya wa Cuba, gazeti la Rheinpfalz la mjini Ludwigshafen linaandika:
"Kwanza kabisa hilo sio jambo jipya mjini Havanna. Jumuiya ya kimataifa na hususan Wacuba wenyewe watalazimika kuwa wavumilivu, wakati rais wao mpya anafahamu matatizo na mahitaji ya kizazi cha vijana , na kujishughulisha nayo kuliko marais waliopita. Pamoja na hayo mageuzi yatakuwa machache na ya juu juu tu kama yatafanyika. Hayatatosha , kuweza kuzuwia kuporomoka."
Hayo ndio kwa muhtasari maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani kama yalivyokusanywa na Sekione Kitojo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman