Maoni ya wahariri
27 Machi 2008
Nishati ni miongoni mwa mahitaji ya msingi ya mwanadamu sawa na chakula na maji.
Na kutokana hayo nishati inapasa kupatikana kwa bei nafuu kwa wananchi wote. Hilo ndilo suala linalozingatiwa leo katika maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.
Wahariri hao wanatoa maoni yao kufuatia pendekezo la mwenyekiti wa chama cha waliberali FDP bwana Guido Westerwelle juu ya kupunguza kodi ya mauzo ili kuifanya bei ya nishati iwe nafuu kwa wananchi wote.
Bwana Westerwelle amependekeza kupunguzwa kodi hiyo kutoka asiliamia 19 hadi asilimia 7.
Lakini gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER halioni hilo kuwa wazo la kufaa sana.
Sababu ni kwamba haitachukua muda kwa makapuni ya nishati kupandisha bei kwa kisingizio cha kuongezeka bei ya nishati kwenye masoko ya kimataifa. Mhariri wa gazeti hilo KÖLNER STADT ANZEIGER anasema kitakachotokea baada ya kuteremsha kodi ya mauzo(VAT) , ni kupungua mapato ya kodi kwenye mfuko wa serikali.
Wazo la kupunguza kodi ya mauzo linapingwa pia na mhariri wa gazeti la WESTFÄLISCHE NACHRICHTEN kutoja mji wa Münster katika jimbo la kaskazini magharibi mwa Ujerumani.
Mhariri huyo anasema pendekezo la mwenyekiti wa chama cha waliberali bwana Westerwelle ni mzaha. Gazeti linasema pendekzo la kupungza bei ya gesi na umeme linavutia lakini alietoa wazo hilo analenga shabaha ya kujijengea umaaruf tu. Mhariri wa gazeti hilo anauliza vipi itawezekana kuziba shimo lililopo katika mfuko wa serikali, ikiwa mapato ya kodi yatapungua?
Mhariri huyo anasema ipo jia moja tu ya kuweza kuondokana na bei za juu za mahitaji ya nishati. Nayo ni kufanya mageuzi kwenye masoko ya nishati hapa nchini Ujerumani.
Lakini mhariri wa gazeti la OFFENBACH POST anasema mtu anaweza kudhihaki pendekezo la mwenyekiti huyo wa chama cha FDP iwapo ataliangalia kijuu juu, lakini akiwa na wasaa wa kulichunguza kwa undani atabaini kuwa,lina maana. Mhariri huyo anauliza kwa nini kiwango cha chini cha kodi ya mauzo kinatozwa katika mapato yanayotokana na mbio za farasi,wakati kodi inayotokana na mauzo ya nepi za watoto ni ya juu.
Gazeti linasema ikiwa kodi ya mauzo itapunguzwa katika gesi na umeme - jambo hilo litaingia akilini. Hatua hiyo ingeleta haki ya kijamii.
Mhariri wa gazeti la PFORZHEIMER anaunga mkono hoja hiyo kwa kusema kuwa bei ya nishati imethibiti kuwa kizingiti kirefu katika ustawi wa uchumi nchini Ujerumani.
Mhariri huyo anasema kila mwananchi anapaswa kumudu kulipia mahitaji yake ya nishati, badala ya nishati kuleta manufaa kwa serikali peke yake.