1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini:Kiongozi wa AfD atoa matamshi ya kibaguzi.

31 Agosti 2017

Magazeti ya Ujerumani yameandika juu ya matamshi ya kibaguzi yaliyotolewa na kiongozi wa chama cha siasa kali cha Afd, Miaka 20 tangu alipofariki Princess Diana wa Uingereza na tufani katika mji wa Texas nchini Marekani.

Deutschland - Britisches Thronfolgerpaar in Celle: Lady Diana
Picha: picture-alliance /dpa/T. Wattenberg

Mhariri wa gazeti la Die Welt la mjini Berlin ameandika juu ya matamshi ya kibaguzi yaliotolewa na kiongozi wa chama cha siasa kali za kizalendo cha AfD cha hapa Ujerumani dhidi ya waziri mwenye asili ya Kituruki. Kiongozi huyo Alexander Gauland,ambaye ni naibu kiongozi wa AfD na mmoja wa wagombea ukansela katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, alisema waziri anaehusika na masuala ya wahamiaji Aydan Özoguz anapaswa kutupwa nchini Uturuki. Juu ya matamshi hayo, mhariri wa Die Welt amesema tatizo ni kwamba Ujerumani imekosa chama halisi cha kihafidhina kwa hiyo haishangazi kwamba jaribio la mwisho la kuunda chama halisi cha kihafidhina nchini Ujerumani limezalisha wanachama wa kuchukiza kama Gauland wa chama cha AfD.

Naye Mhariri wa gazeti la Die Zeit la mjini Hamburg anasema wengi walikuwa na matarajio kwamba Gauland na utu uzima wake baada ya kuchaguliwa kukiongoza chama cha AfD angekuwa mtu wa kujenga utangamano na kwadhibiti wafuasi wenye itikadi kali. Wahariri wa magazeti ya Badische nachrichten na Aachener Zeitung wameandika juu ya kumbukumbu ya miaka 20 tangu kifo cha princess Diana. Mhariri wa Aachener Zeitung anasema kwa umaarufu alioupata katika maisha yake, Diana kama ilivyo kwa watu wengi mashuhuri, angefikia wazo la kujichukulia kuwa muhimu zaidi kuliko alivyokuwa kiuhalisia. Lakini mara zote alitumia umaarufu wake kufanya mambo mazuri. Ukaribu wake na waathirika wa ugonjwa wa ukimwi, waathirika wa mabomu ya kutegwa ardhini, maskini na wagonjwa kwa ujumla, unahitaji tu kutoa heshima wakati wa kumkubuka mwanamama huyu. Zaidi ya yote watoto wake wameliatambua hilo licha ya maumivu ya kumpoteza mama yao wakiwa wadogo. William na Harry wanaendeleza urithi wa mama yao. Kwa uwazi wao na uchangamfu, wao ndiyo taswira ya mama yao - na mustakabali wa Ufalme wa Uingereza.

Mada nyingine ilioangaziwa na wahariri ni juu ya tufani iliyokumba jimbo la Texas nchini Marekani na suala zima la mabadiliko ya tabianchi, Wakati taifa hilo likiongozwa na mtu anayepinga ukweli kuhusu mabadiliko ya tabianchi. Mhariri wa gazeti la EMDER ZEITUNG ameandika juu ya mada hii na kusema. Hata kama Trump angefanikiwa kukabiliana na janga hilo kwa uwezo wake mwenyewe, haipaswi kusahauliwa kwamba ikiwa ataendelea kupinga ukweli kuhusu mabadiliko ya tabianchi, basi yeye ni mmoja wa wahusika wa matukio ya hali ya hewa ya baadaye, kwa maamuzi yake kama vile kujitoa katika mkataba wa mazingira wa Paris hivyo basi Trump anachangia kwenye ongezeko linalotia wasiwasi la majanga ya dhoruba.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Iddi Ssesanga

.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW