Magazetini:Mahakama ya Ulaya imeamua sahihi dhidi ya Hungary
7 Septemba 2017Pia wahariri kadhalika wameandika kuhusu madhila yanayowakuta Waislamu Warohingya nchini Myanmar
Tukianza na gazeti la Rhein Zeitung la mjini Koblenz kuhusu mada ya wakimbizi na wahamiaji mhariri anaandika
Mahakama ya Ulaya imefikia uamuzi sahihi. Mashitaka yaliyotolewa na Hangary katika mahakama hiyo ya Luxemburg yametolewa hukumu ya haki kabisa. Kwasababu haiwezekani kwamba nchi mwanachama linataka kubadilisha uamuzi , ambao inaupendelea tu, na Umoja wa Ulaya hauwezi kufanyakazi kwa njia hiyo na hautafanya hivyo katika siku zijazo. Umoja huu umejengeka katika msingi wa kuwapo tayari kuwa na maridhiano, na ni hilo pekee litaleta maendeleo.
Nalo gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung kuhusu mada hiyo linaandika:
Umoja wa Ulaya ulipitisha azimio kuyasaidia mataifa yaliyoko mstari wa mbele katika mzozo huu wa wakimbizi, Italia na Ugiriki kuwagawa wakimbizi wapatao 120,000 kwenda katika mataifa mengine ya Umoja huo katika muda wa miaka miwili.
Ndipo Hangury na Slovakia , kwa kuungwa mkono na Poland , zilipeleka mashauri katika mahakama ya sheria ya Ulaya kupinga azimio hilo. Ni haki kabisa kwa mujibu wa sheria , kwa mashitaka kama hayo kushindwa.
Gazeti la Badische Neueste Nachrichten la mjini Karlsruhe linazungumzia kuhusu ripoti ya usawa wa kiuchumi nchini Ujerumani baina ya ujerumani mashariki na magharibi. Mhariri anaandika.
Ujenzi wa usawa wa hali ya maisha ni jukumu muhimu sana la majimbo yote nchini Ujerumani. Zaidi ni kuimarisha uwezo wa majimbo yale yenye uchumi dhaifu ili kuzuwia kuporomoka zaidi. Bila hivyo itakuja hali ya mtengano baina ya majimbo yenye hali bora ya kijamii na yale ambayo hali yake ni mbaya. Hii italeta hali mbaya katika amani ya ndani.
Mwishowe ni mada kuhusu madhila yanayowapata Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar. Mhariri wa gateti la Rheinpfalz la mjini Ludwigshafen anaandika.
Kile kinachotokea katika eneo la kaskazini magharibi mwa Myanmar ,kwa kweli ni vigumu kukitathmini. Wachunguzi wasioelemea upande wowote wanazuiwa kuingia katika eneo hilo la machafuko. Lakini kila mzozo huo wa Warohingya unavyoendelea , ndivyo hali inavyozidi kuwa ya wasi wasi zaidi na Waislamu wa Rohingya wanaendelea kukimbilia Bangladesh na katika mataifa mengine ya jirani. Jinsi Myanmar inavyowafanyia Warohingya sio tena mzozo ambao ni wa Myanmar pekee.
Alikuwa sekione Kitojo aliyetukusainyia maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Yusuf , Saumu