Magereza ya Shirika la CIA nchi za nje: Wafungwa kadhaa hawajulikani waliko.
27 Aprili 2009Inaelekea kiasi ya wafungwa 36 waliokua wakishikiliwa katika magereza ya siri ya Shirika la ujasusi la Marekani CIA, katika nchi za kigeni wamepotea na hawajulikani waliko.Jitihada za mashirika yanayotetea haki za binaadamu kujaribu kujua mahala waliko nazo hazikufanikiwa.
Ripoti kuhusu kile kinachoitwa" wafungwa mashetani." ilikusanywa na kukamilishwa wiki iliopita na kundi la uchunguzi la mtandano la waandishi habari linalojulikana kama PRO PUBLICA.
Mwezi Septemba 2007, mkurugenzi wa shirika la ujasusi la Marekani CIA Michael V.Hayden , alisema watu wanaokaribia 100 wamekamatwa na walikua wanazuiliwa katika maeneo yanayosimamiwa na maafisa wa CIA. Taarifa moja iliotolewa hadharani wiki iliopita, ilithibitisha kwamba shirika hilo lilikua likiwazuwia karibu watu 94 hadi kufikia Mai 2005 na likitumia mbinu mbali mbali wakati wa kuwahoji 28 miongoni mwao.
Rais wa zamani George W.Bush aliungama hadharani juu ya mpango huo wa CIA mwezi Septemba 2006, na wafungwa 14 wakahamishwa kutoka magereza ya siri na kupelekwa katika gereza la Guantanamo. Wengi wengine ambao hawakua na umuhimu katika shughuli za usalama kwa jumla, kwa mujibu wa rais Bush wakati huo, walirejeshwa katika nchi zao ili wahukumiwe au waendelee kuzuiliwa na serikali zao.
Lakini Bush hakutaja watu hao walikua ni kutoka nchi gani au mahala walikokuweko, taarifa ambayo ingeliwezesha shirika la kimataifa la msalaba mwekundu kuwatafuta. Pia hakuelezea juu ya masharti ya wafungwa kuzuiliwa katika nchi za kigeni.
Shirika hilo liliweza kuziona na kuziorodhesha nyaraka za watu 14 tu ambao ilifahamika hadharani kwamba walihamishwa na kupelekwa katika gereza la Guantanamo.
Serikali ya Marekani, haikupata kutoa taarifa yoyote inayoelezea hatari inayoweza kusababishwa na wafungwa hao kwa jumla. Baadhi yao wameshaachiwa tangu wakati huo na nchi zilizokua zikiwazuwia, lakini bado haijafahamika wazi nini kimewasibu wengine kadhaa na hakuna serikali yoyote ya kigeni iliokiri kwamba ikiwashikilia kwa niaba ya Marekani.
Mwezi Juni 2007 mashirika yanayotetea haki za binaadamu yalitoa majina ya watu 36 ambao hatima yao haijulikani.
Mwanasheria Gitanjali Gutierrez kutoka kituo cha haki za kikatiba kinachomtetea Majid Khan, mfungwa wa zamani katika gereza la Guantanamo, aliliambia Shirika la habari IPS kwamba sasa utawala wa rais Barack Obama lazima ubadili muelekeo, kwa sababu kuna maswali mengi yasiojibiwa, ikiwa ni pamoja na hili la hatima ya baadhi ya wafungwa waliokua wakishiliwa na Marekani, na waliobandikwa jina la wafungwa mashetani, baada ya kupotea na hadi sasa hakuna ajuawaye mahala waliko.
Hivi karibuni jaji mmoja wa Shirikisho nchini Marekani aliamuru kwamba wafungwa watatu waliokua wakizuiliwa na Marekani katika kambi ya Bagram nchini Afghanistan wanaweza kupinga kuziliwa kwao kisheria katika mahakama za Marekani.Hayo yalitokana na juhudi za kundi la wanasheria wanaotetea haki za binaadamu.
Wafungwa hao waliokamatwa nje ya Afghanistan na ambao si waafghan wamezuiliwa huko Bagram kwa zaidi ya miezi sita sasa bila ya kufunguliwa mashtaka au kupewa haki ya wakili wa kuwatetea. Utawala wa Obama umekataa rufaa kupinga uamuzi wa jaji huyo.
Kundi la Pro Publica limeripoti kwamba afisa mmoja katika utawala wa Bush amesema CIA ilikua mbiyoni mnamo msimu wa joto 2006 kuwahamishia wafungwa katika magereza nchini Pakistan,Misri na Jordan, muda mfupi kabla ya Bush kuungama kuwa shirika hilo lilikua na magerezani nchi za nje na kuusimamisha mpango huo.
Mwanasheria Gutierrez anasema anasema, Marekani ina madaraka ya kutosha kulichunguza shirika lake la ujasusi CIA pamoja na vitendo vya mashirika mengine, kuwaadhibu wale waliokiuka sheria na kuhakikisha taifa hilo halitumbukii tena gizani.
Mwandishi: Abdulrahman, Mohamed/IPS
Mhariri: Josephat Charo