Mageuzi ya Arabuni na nishati ya nyuklia kutawala mkutano wa G8
26 Mei 2011Hotuba ya leo ya Kansela Merkel ilikuwa fupi lakini iliyofumbata kila kitu ndani yake, kutoka msimamo wa Ujerumani kuelekea wimbi la mageuzi katika mataifa ya Kiarabu hadi sera za serikali yake kuelekea nishati ya nyuklia.
"Tunakutana katika wakati ambao kuna wimbi la mageuzi Arabuni na Afrika ya Kaskazini, nasi tunapaswa kuwa na msimamo wa pamoja kuhusu hali hii. Serikali za huko zinajikuta zikilazimika kuakisi matakwa ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi ya watu wao." Kansela Merkel ameliambia Bunge la Ujerumani.
Kama wenzake wa Marekani, Uingereza na Ufaransa, kiongozi huyu wa Ujerumani naye amewapongeza vijana katika mataifa hayo ya Kiarabu kwa ujasiri wao wa kupigania mabadiliko.
Na ingawa si kwa njia ya moja kwa moja, Kansela Merkel naye ametoa hakikisho la msaada wowote unaohitajika kuhakikisha mabadiliko ya kidemokrasia katika mataifa hayo yanaimarika kwa maslahi ya usalama wa ulimwengu mzima.
Kwenye mji wa Deauville wenyewe, ambako mkutano huu unafanyika, hali ya usalama inaripotiwa kuimarishwa, ambapo zaidi ya polisi 10,000 wamemwagwa kwenye kila pembe ya mji huo wa ufukweni. Hata ile kawaida ya kuwepo kwa maandamano kila mkutano wa aina kama hii unapofanyika, safari hii inaonekana kukiukwa.
Mkutano huu hautajadili suala la wimbi la mageuzi ya Arabuni tu, bali pia usalama katika mitandao ya kompyuta, ambao kwa siku za karibuni umekuwa ukikumbwa na aina mbali mbali za uhalifu na pia suala zima la nishati ya nyuklia.
Hili linatiliwa mkazo na hali ya mmoja wa wanachama wa G8, Japan, ambayo ilikumbwa na janga la tetemeko la ardhi na tsunami mwezi Machi mwaka huu, na kuviathiri vibaya vinu vya nyuklia vya Fukushima nchini humo. Hili ndilo analokwenda nalo Waziri Mkuu wa Japan, Naoto Kan.
"Nitaelezea namna ambavyo Japan imepambana na inavyohitaji msaada wa kupambana na athari za janga hili. Hilo ndilo nitakalouomba ulimwengu na marafiki zetu wa G8." Amesema Kan.
Rais Nicolas Sarkuzy, ambaye nchi yake inaongoza barani Ulaya kwa kuwa na vinu vingi vya nyuklia, naye pia anatafuta kuwa na sera ya pamoja ya usalama wa vinu hivyo katika mataifa ya G8.
Juu ya hayo, kuna suala pia la mrithi wa nafasi ya ukuu wa Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF, baada ya Mfaransa Dominique Strauss-Kahn, kujiuzulu akikabaliwa na kesi ya ubakaji.
Jumuiya ya G8 inayoyaleta pamoja mataifa tajiri sana duniani, ina usemi mkubwa kwenye hatima ya Shirika hilo na ingelipenda kuona kuwa mtu anayechukuwa nafasi hiyo, ni yule anayekubalika kwao.
Tayari Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, ametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo, akiwa na uhakika wa uungwaji mkono wa mengi ya mataifa yaliyomo kwenye G8, ikiwemo Ujerumani, ambayo tangu mwanzo Kansela Merkel alishasema kwamba, angelipenda kuona mrithi wa Strauss-Kahn anatokea kwenye Umoja wa Ulaya.
Suala la uchangiaji wa Shirika hilo la Fedha la Kimataifa linatarajiwa pia kujadiliwa kwa kina, ambapo hadi sasa, mataifa haya ya G8 yanakisiwa kuchangia karibu asimilia 50 ya mfuko wa taasisi hiyo yenye usemi mkubwa sana kwenye uchumi wa ulimwengu, na hivyo kuyapa mataifa hayo kauli ya juu.
Mwandishi: Andreas Reuter/ZPR
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Josephat Charo