Mageuzi ya Katiba kutiwa saini Pakistan
19 Aprili 2010Mageuzi hayo yatamaliza ukiukaji wa katiba uliokuwa ukifanywa na viongozi wa kijeshi kwa miongo minne iliyopita na yatamnyanganya kiongozi wa taifa madaraka yanayomwezesha kumfukuza kazi waziri mkuu, kuwachagua wakuu wa jeshi na kuvunja bunge. Kuambatana na mageuzi hayo ya katiba, Waziri Mkuu Yousuf Raza Gilani atakuwa na mamlaka ya uongozi. Hatua hiyo huenda ikasaidia kuleta utulivu wa kisiasa na kupunguza mivutano katika nchi inayomiliki silaha za nyuklia na iliyo mstari wa mbele kupigana dhidi ya ugaidi katika vita vinavyoongozwa na Marekani.
Mwezi huu, mabunge yote mawili ya Pakistan yaliidhinisha mswada wa sheria itakayomaliza utaratibu uliokuwa ukitumiwa na serikali za kijeshi kudhoofisha katiba ya bunge ya mwaka 1973. Mageuzi yanayotiwa saini na Rais Zardari, yatafutilia mbali madaraka waliyojikusanyia madikteta wa kijeshi Pervez Musharraf na Zia ul Haq. Lakini jeshi litaendelea kuwa na nguvu nchini Pakistan ambako vikosi vya serikali vinapigana na wafuasi wa Taliban na Al Qaeda.
Mswada huo wa sheria unaotiwa saini leo mchana katika ofisi ya rais, kwenye sherehe itakayohudhuriwa pia na kiongozi maarufu wa upinzani Nawaz Sharif, vile vile utaondoa kipengele kinachomzuia waziri mkuu kugombea wadhifa huo kwa zaidi ya awamu mbili. Kwa hivyo, Nawaz Sharif aliengolewa madarakani na Pervez Musharraf katika mwaka 1999, sasa ataruhusiwa kugombea uchaguzi kuwa waziri mkuu mara nyingine tena.
Juma lililopita, Waziri Mkuu wa Pakistan Gilani aliusifu mswada wa mageuzi ya katiba kama ni ushindi kwa demokrasia. Amesema, hiyo ni hatua muhimu ya kihistoria katika katiba ya Pakistan. Kuambatana na marekebisho hayo ya katiba, Rais Zardari atakuwa na cheo cha kiongozi wa taifa, atakaeweza kuwateua viongozi wa majeshi, kuvunja bunge la taifa na kuwateua magavana wa majimbo baada tu ya kushauriwa na waziri mkuu.
Kuidhinishwa kwa mswada huo kumesifiwa kama tukio lililoweka kando tofauti zilizokuwepo kati ya vyama mbali mbali katika nchi yenye mivutano mikali ya kisiasa. Lakini wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaonya kuwa mageuzi hayo hayatosaidia hivyo matatizo ya kila siku yanayoikabili nchi hiyo. Zardari ataendelea kuwa na ushawishi katika maamuzi ya kisiasa kwa sababu yeye ni kiongozi wa chama tawala. Hicho ni cheo alichorithi baada ya mke wake, Benazir Bhutto aliekuwa waziri mkuu mara mbili, kuuawa Desemba 2007.
Mwandishi:Martin,Prema/AFPE
Mhariri: M.Abdul-Rahman