1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaKorea Kusini

Mageuzi ya kisera ya Pyongyang kuzitenga zaidi Korea mbili?

5 Januari 2024

Korea Kaskazini inaonekana kuchukuwa muelekeo mpya kwenye mahusiano yake na Korea Kusini kwa kuanzisha mabadiliko kwenye sera na mashirika ya serikali ambayo yanaweza kuigeuza Kusini kuwa dola la mbali na adui.

Korea Kaskazini | Majaribio ya silaha nzito
Mpango wa makombora ya masafa wa Korea Kaskazini umekuwa chanzo cha mivutano kwenye rasi ya Korea Picha: YNA/picture alliance

Hatua hiyo ambayo inavunja sera iliyokuwapo kwa miongo mingi sasa, inaweza kuipa fursa wizara ya mambo ya kigeni ya Korea Kaskazini kuwa jukumu la mahusiano yake na Kusini, jambo linaloweza kuhalalisha matumizi ya silaha za nyuklia dhidi ya Seoul, endapo kutakujazuka vita baina yao.

Tangu kumalizika kwa Vita vya Korea vya mwaka1950-53, kila nchi kati ya hizo mbili imekuwa na sera zinazoichukulia nyengine kwa namna tafauti na vile zinavyohusiana na mataifa ya kigeni.

Kwa ufupi, Korea zote mbili zinachukuliana kuwa na ndugu wawili waliogombana tu na sio kwamba ni mataifa mawili jirani ya kigeni.

Hilo linajumuisha kuwa na mashirika maalum ya pamoja na wizara za kushukilia masuala ya Korea badala ya kuwa na wizara za mambo ya kigeni, na kukumatia sera kwa ajili ya kuungana tena katika siku zijazo, ambapo itakuwa tena nchi moja lakini yenye mifumo miwili tafauti ya utawala.

Matamshi ya Kim Jong Un yakoleza moto mivutano rasi ya Korea

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong UnPicha: KCNA/REUTERS

Kwenye hotuba ya kufungia mkutano wa mwisho wa mwaka wa chama chake, kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, alisema "kuziiunganisha tena nchi hizo kwa amani ni jambo lisilowezekana" na badala yake akatangaza kuwa serikali yake itafanya mabadiliko makubwa ya kisera kwenye mahusiano yake na adui.

Kiongozi huyo aliamuru pia jeshi kuwa tayari kuitwaa na kuikalia Kusini ikiwa kutazuka mzozo baina yao.

Mabadiliko hayo ya sera yanaweza kuisaidia Korea Kaskazini kupata uhalali wa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya Kusini, kama ambavyo imekuwa ikitishia katika miaka ya hivi karibuni, anasema Hong Min, mtafiit wa ngazi za juu wa Taasisi ya Muungano wa Kitaifa ya Korea mjini Seoul.

Hong ameongeza na hapa namnukuu: "Endapo wataachana na suala la muungano wa amani na kuiweka Korea Kusini kwenye kundi la mataifa hasimu lisilo na mahusiano ya kidiplomasia, ule utata wa kutumia silaha za nyuklia dhidi ya ndugu zako utakuwa umeondolewa." Mwisho wa kumnukuu.

Wachambuzi wengine wanasema tangazo hilo la Korea Kaskazini linaakisi tu uhalisia wa nchi mbili zenye migawanyiko na mitafaruku ya ndani.

Rachel Minyoung Lee wa Kituo cha Stimson chenye makao yake makuu nchini Marekani, anasema katika miaka ya karibuni, Pyongyang ilishaashiria kwamba ilikuwa inaelekea kwenye mabadiliko makubwa ya kisera kuelekea Kusini, na kile kilichosemwa kwenye hafla ya chama cha Kikomunisti ya Disemba 2023 kilikuwa kinayarasmisha tu mabadiliko hayo.

Kipi kipya katika mageuzi ya sasa ya kisera ya Pyongyang?

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un akiagana na rais wa wakati huo wa Korea Kusini Moon Jae-In pamoja na aliyekuwa rais wa Marekani wakati huo Donald Trump baada ya mkutano wao wa kihistoria kwenye mpaka baina ya Korea mbili mnamo mwaka 2019.Picha: KCNA/AP Photo/picture alliance

Bado haijawa wazi ikiwa mageuzi ya kimuundo yatafika umbali gani, lakini kwa kuzingatia kuwa kauli kama hizi zinaakisi tu hali ambayo tayari ipo, huenda mageuzi hayo yasiwe na uzito wowote kwenye mahusiano ambayo tayari yameshakuwa ya kiadui kati ya Korea hizo mbili.

Wakati kulipotokea hali ya wasiwasi mkubwa baina ya pande hizo mbili, kama vile mwaka 2016 na 2017, vilikuwa vikifuatiliwa na juhudi za kidiplomasia kama vile mikutano ya kilele ya Kim na marais wa Korea na Marekani.

Taarifa ya wizara ya muungano ya Korea Kusini ilisema kwamba ingawa Korea Kaskazini imesema haitaizingatia tena wizara  hiyo kuwa mshirika wa kuzungumzia muafaka na muungano, lakini ukweli ni kuwa kamwe haijawahi kuichukulia Korea Kusini kwa namna hiyo.

Hiyo ni kusema tangazo la Kim si jambo jipya.