1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magofu ya kihistoria Bagamoyo hatarini kutoweka

Christopher Buke7 Agosti 2006

Hayatunzwi ipasavyo, huku baadhi ya vitu vikiibwa

Kila kabila au kila jamii ya watu huwa na misemo yao. Huitumia misemo hiyo kuonyesha furaha yao, kuonya au kufundisha jamii juu ya masuala mbalimbali. Waswahili nao wana misemo yao. Moja wapo ya misemo hiyo ni pamoja na “Kitunze kidumu” au “Kitunze kikutunze”!

Msemo huu kwa hakika unapaswa kuzingatiwa na Sekta ya Utalii nchini Tanzania hasa baada ya mabingwa wa mambo ya kale na utalii kuonya hivi karibuni kuwa magofu ya kihistoria na ambayo ni miongoni mwa vivutio muhimu vya utalii yamo hatarini kuharibika na kutoweka.

Uharibifu huu unatokana na sababu mbalimbali kama vile kutokana na wakati, baadhi ya vitu kwenye magofu hayo vinaibwa, vinaharibiwa wakati magofu mengine yakizidi kuchakaa na kubomoka kutokana na kutokarabatiwa.

Magofu yanayokabiriwa na kitisho hiki hasa ni ya Mji mkongwe wa Bagamoyo ambao hivi sasa unaratibiwa kuwa sehemu ya Urithi wa Dunia.

Ni kutokana na hali hiyo wadau wa sekta ya utalii Idara ya Utunzaji wa Mambo ya Kale wameanza kuweka mikakati kuhakikisha urithi huu unatunzwa. Mikakati hii ni pamoja na kuwakutanisha wadau wa mkongo huu (Claster) wa utalii ili yakusanywe maoni na mapendekezo.

Katika mada mbalibali zilizowasilishwa katika warshsa ya namna hii kwa mfano iliyofanyikia mjini Bagamoyo July 27, 2006 wadau walishauri mambo kadha wa kadha yazingatiwe na kuangaliwa kwa ukaribu na wadau wa wa sekta ya Utalii ambao ni serikali na jamii hasa ya wakazi wa Bagamoyo.

Lakini pia hata mashirika mbalimbali ya kimataifa, taasisi za kiserikali na zile zisizo kuwa za kiserikali zimeanza kuhamasisha umuhimu wa kutunzwa magofu haya.

Taasisi hizo ni pamoja na CoeT, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Shirika la Ushirikiano wa Misaada wa Maendeleo la Sweden SIDA, SAREC na VINNOVA ya Sweden.

Katika kongamano nililotangulia kulitaja washiriki pia walitoa mwito wa kuishirikisha kikamilifu jamii ya wakazi wa Bagamoyo, katika kupanga na kuamua mikakati madhubuti badala ya kupewa taarifa za baadhi ya maadhimio ambayo hupitishwa bila ya wao kuhusishwa.

Baadhi ya maazimio yaliyopitishwa ni pamoja na kuufanya mji wa Bagamoyo kuwa kituo cha watalii wa ndani na nje ya nchini katika kipindi cha miaka miaka mitano ijayo.

Wakataka waongozaji wa watalii (tourguides) waongezewe elimu ili waendeshe kazi hiyo kwa ufanisi zaidi. Hii ni pamoja na kuwapatia nyenzo na vitendea kazi.

Azimio lingine lilikuwa kutaka suala la usalama wa watalii lizingatiwe zaidi. Hii kutokana na washiriki hao kuwa na wasiwasi na baadhi ya maeneo wanayodhani hakuna dalili za kuwepo usalama kwa raia na watalii hususan nyakati za usiku.

Lingine ni kuwawezesha watalii kufika katika mbuga ya wanyama ya Saadani kupitia Bagamoyo na kisha Makurunge kwa kutumia boti.

Mkakati mwingine ni kutaka juhudi zaidi ziongezwe za kuweka na kudumisha mawasiliano na Zanzibar (ambayo tayari ni kituo cha utalii), ili kuleta ongezeko la wataliii, hasa wale watakaopenda kutembelea sehemu za historia ya utamaduni pamoja na mbuga za wanyama.

Mkutano huu pia ukaazimia kuwa wawakilishi katika sekta ndogo za utalii wawe ni Hoteli za kitalii, Nyumba za kulala wageni, Sanaa na wasanii, Mila na desturi, Waongozaji wa watalii, Taasisi za elimu, Serikali na taasisi zake, Usafiri na usafirishaji na Waandaaji wa vyakula.

Mji mkongwe wa Bagamoyo unakadiriwa kuanza kutukuka mwishoni mwa 1800 AD. Chimbuko la mji huu ambako sasa panajulikana kama eneo la magofu ya Kaole, kadri ya kilomita tano kutoka mji wa sasa wa Bagamoyo.

Kabla ya hapo Kaole ilikuwa bandari muhimu katika pwani ya Afrika Mashariki. Umuhimu wake ukihusishwa na biashara ya masafa marefu baina ya mlima Hinterland na mabara ya Asia, Arabia na Mashariki ya mbali ilhali na bidhaa kama za pembe za ndovu, ngozi za simba, ngozi za chui, vyombo vya kauli, shanga pamoja na bidhaa nyingine toka ng’ambo.

Mnamo mwishoni mwa karne ya kumi na nane makazi hayo ya Kaole yakahamia mji wa sasa wa Bagamoyo kutokana na sababu mbalimba za kijamii, kiuchumi na kimazingira.

Kwa hiyo kati ya mwaka 1800 hadi 1830 Bagamoyo iliweza kukua na kuchukua nafasi ya Kaole kama bandari kuu, kituo muhimu cha biashara na sehemu iliyokuwa inaendelea katika kilimo na uvuvi. Bandari hii ikaziunganisha nchi na mabara.

Ikumbukwe pia kuwa Wajerumani wakaifanya Bagamoyo kuwa makao yao makuu ya utawala katika Afrika ya Mashariki ambayo baadae yalikuja kuhamishiwa Dar es salaam mwaka 1891.

Inajulikana kwa walio wengi kuwa kutokana na wageni hawa, biashara mbalimbali, ushawishi wa kisiasa kutoka nchi mbalimbali duniani na mapokeo ya wenyeji vilichangia pakubwa kupatikana utamaduni ambao baadhi leo hii wakiuita uswahili au utamaduni wa Pwani.

Lakini zaidi utamaduni huu ukichangiwa mno na mchanganyiko na ushawishi wa Kiarabu, Kihindi na Kijerumani.

Shughuli zote hizi, heka heka za kimaendeleo na kadhalika zilipelekea kujengwa majengo yaliyokuwa yakitumiwa katika shughuli mbalimbali ambayo sasa yamebaki kama magofu.

Ama kwa upande mwingine magofu haya yamegeuka kuwa rasilimali muhimu katika sekta ya utalii lakini pia kuwanufaisha wakazi wa Bagamoyo.

Mengi ya magofu haya yapo katika hifadhi ya mji mkongwe wa Bagamoyo ingawa sio mahame bali eneo hili linatumiwa kama makazi ya watu, sehemu za biashara, ofisi za serikali na mashirika mbalimbali.

Watalii hupita kwenye magofu haya wakiyachungulia baadhi wakiyapiga picha, kando kando ya barabara nyembamba na kando ya ufukwe wa bahari ya Hindi.

Ufundi na usanifu majengo katika mji huu mkongwe ulitokana na pande hizo nne nilizo tangulia kuzitaja yaani Wajerumani Waarabu Wahindi na kwa sehemu ndogo Wenyeji.

Vivutio hivi vya kitalii katika mji huu vimetengwa katika mafungu mawili, la kwanza likiwa ni vivutio vya asili ( natural attractions) na vile ambavyo ni matokeo ya kazi za binadamu na vya utamaduni (cultural Attractions).

Vivutio vya asili ni pamoja na uoto wa asili, mfano mikoko, fukwe safi na za kuvutia, uoto wa baharini (sea gardens) samaki na viumbe wengine wa baharini na bahari yenyewe ambayo baadhi wakipenda kuketi fukweni wakielekeza nyuso zao vilindini na kupunga upepo lakini hata kuogelea.

Vivutio vya utamaduni ni kama magofu, majengo ya kale na ya kihistoria, mila na desturi, maeneo ya kihistoria, imani za dini mbalimbali, Imani za kitamaduni na kishirikina, Taasisi zinazojihusisha na masuala ya utamadni kama Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo, makumbusho pamoja na Nyumba za Ibada kama vile Makanisa na Misikiti ya kale.

Vigezo vilivyotumiwa kuainisha majengo ya kihstoria ni kutokana na Sheria ya Mambo ya Kale ya mwaka 1964 pamoja na marekebisho yake ya mwaka 1979. sheria hii inayatambua majengo yote yaliyojengwa kabla ya mwaka 1863 hasa yenye usanifu wa Kiarabu Kihindi Kijerumani na Kitamaduni kuwa yamestahiki kuwa ya kihistoria.

Majengo yenye usanifu wa kiarabu ni kama jengo la Dotoo iliyokuwa ofisi ya mkuu wa wilaya posta ya zamani, Msikiti wa Jamatini, nk. Yale yenye usanifu wa kihindi ni pamoja na majengo yaliyo mtaa wa India, Caravan Serai, Naser virji nk.wakati majengo yenye usanifu wa Kijerumani ni pamoja na boma, jengo linalotumiwa hivi sasa na Ushuru wa Forodha.

Lakini kuna majengo yenye usanifu usio elemea pande hizi au yakiitwa yenye usanifu mchanganyiko ambayo ni mgahawa wa kiarabu (Arab TeA House) majengo yaliyoko eneo la Kanisa Katoliki, yale yanayotumiwa kama shule mchanganyiko ya Mwambao, jengo la Hospitali ya kwanza eneo la hospitali ya wilaya.

Mwisho.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW