1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli aapishwa rasmi kuwa rais wa Tanzania

Admin.WagnerD5 Novemba 2015

John Pombe Magufuli ameapishwa kuwa rais wa awamu ya tano wa Tanzania, katika sherehe zilizofanyika uwanja wa Uhuru mjini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na maelfu ya raia pamoja na viongozi wengii wa nchi za kiafrika

Tansania Amtseid Präsident John Magufuli
Picha: Reuters/E. Herman

Dakta John Pombe Magufuli amekula kiapo cha kuanza rasmi majukumu kama rais mpya wa Tanzania. Kiapo hicho kilitanguliwa na utaratibu maalumu wa kukabidhiana madaraka, ambapo rais wa awamu ya nne wa Tanzania Jakaya Kikwete aliwaaga raia wa Tanzania, na kisha bendera yake kushushwa, kuipisha ile ya rais wa awamu ya tano.

Hali kadhalika makamu wa rais Samia Suluhu Hassan pia amekula kiapo chake na kuahidi kumpa ushauri wa busara rais Magufuli. Yeye ni mwanamke wa kwanza katika historia ya Tanzania kuwa makamu wa kwanza wa rais wa Jamhuri ya muungano.

Kiapo cha rais Magufuli kimesimamiwa na jaji mkuu wa Tanzania Othman Chande na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano Anna Makinda, pamoja na viongozi wa kidini. Baada ya hapo rais mpya amekabidhiwa na wazee ngao na mkuki kama alama za uongozi, na kisha akakagua gwaride la kijeshi kupokea heshima kama amiri jeshi mkuu. Mizinga ishirini na moja ilifyatuliwa kwa heshima yake, huku ndege za kijeshi zikipaa katika anga ya viwanja zilikofanyika sherehe hizo.

Makamu wa rais Tanzania, Samia SuluhuPicha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Viongozi kadhaa wahudhuria

Viongozi kadhaa kutoka nchi jirani ya Tanzania na za mbali barani Afrika walikuwepo kushuhudia shughuli hiyo. Miongoni mwao ni Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, wa Rwanda Paul Kagame, na wa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Kongo Joseph Kabila.

Hali kadhalika sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, wa Zimbabwe Robert Mugabe, Rais wa Msumbiji Filepe Nyusi na wa Waziri Mkuu wa Ethiopia Hailemariam Desalegn.

Rais wa Zanzibar Ali Mohammed Shein ameshiriki katika sherehe hizo, ingawa bado hatima ya uchaguzi visiwani Zanzibar inakumbwa na sintofahamu, baada ya tume ya uchaguzi visiwani humo kuyafuta matokeo kwa madai ya kuwepo hila za udanganyifu.

Upinzani wamesusia

Upinzani ambao haukutambua ushindi wa, John Magufuli, haukuhudhuria sherehe hizo. Kwa mujibu wa mwandishi wa DW mjini Dar es Salaam, George Njogopa, mgawanyiko huo wa maoni kisiasa unadhihirika pia mitaani, ambapo hakuna hali ya shamra shamra iliyozoeleka wakati kama huu wa kumuapisha rais mpya.

Mwandishi: Daniel Gakuba

Mhariri:Yusuf Saumu

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW