1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli afariki dunia akiwa na umri wa miaka 61

18 Machi 2021

Akilihutubia taifa usiku wa Machi 17, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alisema Magufuli alifariki majira ya saa 12:00 jioni kutokana na tatizo la moyo.

Tansania Präsident John Magufuli verstorben
Picha: AFP

Kiongozi huyo aliyepewa jina la "tingatinga" kwa jinsi alivyojipambanuwa kama mpambanaji dhidi ya ubadhirifu kwenye sekta ya umma, amefariki baada ya wiki kadhaa za fununu kwamba alikuwa ameambukizwa virusi vya corona, ingawa taarifa rasmi ya serikali kupitia kwa Makamu wa Rais, Bi Samia Suluhu Hassan, ilisema kuwa alifariki kwa matatizo ya moyo.

Watu wengi watamkumbuka kwa namna alivyolishughulikia kwa utata janga hilo.

Mara ya mwisho kiongozi huyo wa taifa hilo la Afrika Mashariki kuonekana hadharani ilikuwa tarehe 27 Februari. Maafisa wakuu serikalini awali walikanusha kuwa rais anaumwa, ingawa kulikuwa na uvumi kuwa anauguwa na alikuwa hali mahututi.

soma zaidi:Yuko wapi Rais Magufuli?

Rais Magufuli alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliokuwa hawaamini uwepo wa ugonjwa wa COVID-19. Mwaka uliopita alisema Tanzania ilifanikiwa kupambana na kuudhibiti ugonjwa huo kupitia siku tatu za maombi. 

Tanzania haijaripoti visa au vifo vitokanavyo na corona tangu mwezi Aprili 2020. Lakini idadi ya vifo vya watu wanaokufa kutokana na matatizo ya kupumua iliongezeka mapema mwaka huu.

Utata kuhusu COVID-19

Kikao cha mwisho kati ya Rais Magufuli (kulia) na Makamu wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad, mjini Chato mnamo tarehe 14 Januari 2021. Wote wawili sasa ni marehemu. Picha: State House, Dar es Salaam

Ubalozi wa Marekani ulionya juu ya kuongezeka maradufu kwa idadi ya watu wanaougua COVID-19 nchini humo kuanzia mwezi Januari.

Ilikuwa ni hadi baada ya kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad kutokana na virusi hivyo vya corona, ndipo Rais Magufuli na Watanzania walio wengi walianza polepole kukiri uwepo wa virusi hivyo nchini.

soma zaidi: Lissu asema Magufuli amehamishiwa India akiugua Covid-19

Maalim Seif alifariki tarehe 17 Februari, mwezi mmoja kamili uliopita.

Baadaye wizara ya afya nchini humo ilitoa maelezo kwa wananchi kuzingatia masharti ya kupambana na virusi vya corona.

Wakosoaji wanasema kupuuza kitisho cha virusi vya corona kulikofanywa na Marehemu Magufuli pamoja na kukataa kuweka masharti na kuchukua hatua za kuvidhibiti virusi hivyo kama yalivyofanya mataifa mengine huenda ikawa kumechangia vifo vingi nchini humo kikiwemo kifo chake mwenyewe.