1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magufuli azindua reli ya kiwango cha kimataifa

12 Aprili 2017

Kwa mara ya kwanza, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua ujenzi wa reli ya kiwango cha kimataifa itakayotumia umeme unaotarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 30 kuanzia sasa. 

John Magufuli of Tanzania
Rais John Magufuli, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa reli ya viwango vya kimataifa jijini Dar es Salaam 12.04.2017Picha: DW/G.Njogopa

Uzinduzi huo ni awamu ya kwanza inayoanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na baadaye awamu ya pili itaingia makao makuu ya taifa hilo la Afrika Mashariki, Dodoma, na mikoa mingine ikiwamo ile iliyoko katika maeneo ya mipakani.

Uzinduzi huo umefanywa na Rais John Magufuli ambaye amesema hii ni mara ya kwanza kwa nchi yake kugharamikia usafiri wa reli ya kiwango cha kimataifa ikigharimiwa na fedha za ndani. 

Itakapokamilika, reli hiyo itakuwa ni habari njema kwa wakaazi wa Morogoro na Dar es Salaam, ambapo Rais Magufuli amesema sasa "watakuwa wanaweza kuishi mji mmoja na kufanya kazi mji mwengine" na watakuwa na urahisi wa kusafiri kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa muda mfupi.

Abiria wanaosafiri kwa basi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro walikuwa wanatumia muda wa masaa matatu, lakini kutokana na vizuizi vilivyoongezwa na kikosi cha usalama wa barabarani, safari hiyo sasa inachukua hadi muda wa masaa manne hadi matano. 

Reli nyingine nchini humo, kama ile inayoiunganisha na Zambia (TAZARA) na ile inayoiunganisha Dar es Salaam ni mikoa ya ndani (Reli ya Kati), ziligharamikiwa na nchi wahisani.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli kwenye uzinduzi wa reli hiyo, "kutumia fedha za walipa kodi ni hatua ambayo inamulika uwezo wa baadhi ya nchi za Afrika kugharimia miradi mikubwa ya maendeleo bila kutegemea wahisani."
Reli hiyo mpya ambayo inafanana na ile iliyozinduliwa hivi karibuni nchini Kenya, lakini Kenya ikitumia mkopo kutoka China itakuwa mkombozi kwa mataifa mengi yanayopakana na Tanzania. 

Kwa maana hiyo wananchi wa nchi kama Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Rwanda, Zambia, Uganda na hata Sudan Kusini watakuwa na maingiliano ya karibu ya kibiashara hatua ambayo inaweza kutoa msukumo mpya wa kiuchumi kwa nchi za Afrika. 

Rais John Magufuli, katikati, na waziri wake wa ujenzi, Makame Mbarawa, wakati wa uzinduzi wa reli jijini Dar es SalaamPicha: DW/G.Njogopa

Kwa sasa, Tanzania iko katika mpango wa kuboresha sekta ya nishati ya umeme, ikiwamo mradi unaoendelea wa kutegemea gesi ya Mtwara. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa kuna mengi yatakayohitaji kufanywa ili mradi huo uwe endelevu. 

"Huenda tatizo la kukosekana kwa nishati ya uhakika lisiwe tatizo kubwa, lakini jambo linalotia wasiwasi ni kukosekana kwa utashi wa kweli kuendeleza miradi iliyoko," anasema Ludger Kasumuni, mchambuzi wa masuala ya uchumi na maendeleo. 

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam
Mhariri: Josephat Charo
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW