Mahakama haitorudisha marufuku ya Trump
5 Februari 2017Hukumu hiyo imezidi kumpa pigo Trump ambaye amemshutumu jaji katika jimbo la Washington aliyezuwiya amri yake hiyo hapo Ijumaa.Katika kauli alizotowa kwenye mtandao wa Twitter na kwa waandishi wa habari rais huyo amesisitiza atairudisha marafuku hiyo.
Trump amesema marufuku hiyo ya safari ya siku 90 kwa raia wanaotoka Iran,Iraq,Libya, Somalia,Sudan,Syria na Yemen na kupigwa marufuku kwa wakimbizi kuingia nchini humo kwa siku 120 inahitajika kuilinda Marekani dhidi ya wanamgabo wa Kiislamu wa itikadi kali.Wakosoaji wanasema hatua hizo sio za haki na zinabaguwa.
Hukumu ya jaji ya kuzuwiya marufuku hiyo na hukumu ya rufaa imeleta kile kinachoweza kuwa fursa ya muda mfupi kwa wasafiri kutoka nchi saba zilizoathirika kuingia nchini Marekani wakati mashaka ya kisheria yakiendelea.
Mwanamke wa Yemen amekaririwa akisema "Hii ni mara ya kwanza najaribu kusafiri kwenda Marekani.Ilikuwa tumepangiwa kusafiri wiki ijayo lakini tumeamuwa kusogeza mbele baada ya kusikia hayo.Mwanamke huyo
aliefunga ndoa na raia wa Marekani hivi karibuni amepanda ndege kutokea Cairo kuelekea Uturuki hapo Jumapili kuunganisha safari na ndege inayoelekea Marekani. Amekataa kutaja jina lake kwa hofu kwamba itatatiza kuingia kwake nchini Marekani.
Katika amri fupi mahakama hiyo ya rufaa nchini Marekani imesema ombi la serikali la kutaka kusitishwa mara moja uamuzi wa jaji wa Marekani limekataliwa.Inasubiri kuwasilishwa kwa rufaa zaidi kutoka majimbo ya Washington na Minnesota Jumapili na kutoka kwa serikali Jumatatu.
Vikwazo vya usafiri yilivyotangazwa na Trump hapo Januari 27 vimezusha shutuma kutoka kwa washirika wa Marekani na kusababisha vurugu kwa maelfu ya watu ambao katika baadhi ya kesi wametumia miaka mingi kutafuta hifadhi nchini Marekani.
Katika hukumu yake kwenye jimbo la Washington hapo Ijumaa Jaji James Robert amehoji kutumia mashambulizi ya Septemba 11 2001 nchini Marekani kuhalalisha marufuku hiyo kwa kusema hakuna mashambulizi yaliofanywa katika ardhi ya Marekani na watu kutoka katika nchi hizo saba tokea wakati huo.
Mashambulizi ya Septemba 11 yalifanywa na wateka nyara kutoka Saudi Arabia Umoja wa Falme za Kiarabu,Misri na Lebanon ambao raia wake hawakuathirika na marufuku hiyo.
Katika taarifa kadhaa kwenye mtandao wa Twitter hapo Jumamosi Trump ameshambulia maoni ya huyo "anayejiita jaji"kuwa ni upuuzi.Trump amewaambia waandishi wa habari katika eneo lake binafsi la mapumziko la Mar-a-Lago huko Florida "Tutashinda.Kwa usalama wa nchi tutashinda."
Ombi hilo la Wizara ya Sheria limeshutumu hoja ya kisheria ya Robert kwa kusema inakiuka utengeneshaji wa madaraka na kuingilia mamlaka ya rais kama amiri jeshi.
Hata hivyo hukumu hiyo ya mahakama ya Washington ni hatua ya kwanza kwa kile kinachoweza kuwa changamoto za kisheria zitakazodumu kwa miezi mingi kushinikiza kubanwa kwa wahamiaji.Rufaa hiyo inasema jimbo la Washington halina msimamo wa kupinga amri hiyo na imekanusha kwamba inawapendelea Wakristo dhidi ya Waislamu.
Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters
Mhariri : John Juma