Mahakama ya Katiba Kongo yaidhinisha ushindi wa Tshisekedi
9 Januari 2024''Bwana Tshisekedi Tshilombo Felix Antoine amechaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa wingi wa kura zilizopigwa,'' alisema Kamuleta Badibanga Dieudonne, Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba nchini Kongo.
Awali, Mahakama ilitupilia mbali hoja ya mgombea wa upinzani Theodore Ngoy yakutaka uchaguzi urudiwe, mahakama ilisema hoja hiyo haina msingi. Ngoy ambaye alipata chini ya asilimia moja ya kura, ndiye mgombea pekee aliyekata rufaa.
Upinzani kuendelea kupinga matokeo ya uchaguzi
Baadhi ya wagombea wengine wa urais wakiwemo Moïse Katumbi, Martin Fayulu na Denis Mukwege wao wametaka matokeo ya uchaguzi yabatilishwe lakini walikataa kufungua shauri mahakamani wakadai chombo hicho kinaendesha kazi zake kwa misingi ya upendeleo. Wanalalamika kuwa uchaguzi huo mkuu uligubikwa na hitilafu nyingi na matokeo yake yalikuwa ya udanganyifu.
Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 60, ataapishwa mwishoni mwa mwezi huu wa Januari kwa muhula wa pili wa miaka mitano.