1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kenya yabatilisha muswada wa fedha wa 2023

Sylvia Mwehozi
1 Agosti 2024

Mahakama ya Rufaa nchini Kenya imebatilisha muswada tata wa fedha wa 2023 ambao ulisainiwa mwaka jana, na kuongeza masaibu kwa Rais William Ruto anayekabiliwa na mzozo wa uhaba wa fedha katika utawala wake.

William Ruto
Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Hukumu hiyo ya mahakama inafuatia uamuzi wa rais Ruto mwezi uliopita wa kuufutilia mbali muswada tata wa fedha wa 2024 ambao ulichochea maandamano makubwa ambayo wakati mwingine yaligeuka kuwa ya vurugu kuhusu ongezeko la ushuru katika rasimu ya muswada huo.

Majaji watatu wa mahakama ya rufaa wamebaini kwamba sheria hiyo ya fedha ya mwaka 2023 "kimsingi ilikuwa na dosari na hivyo ni kinyume na katiba" kwa sababu ya kushindwa kwa taratibu za bunge.

Ruto aliusaini muswada wa fedha wa 2023 kuwa sheria mnamo mwezi Juni mwaka uliopita, katika juhudi za kukusanya zaidi ya dola bilioni 2.1 na kusaidia kupunguza gharama kubwa za ulipaji wa madeni nchini Kenya.IGP Kenya ajiwajibisha kwa vifo vya waandamanaji

Waandamanaji waongeza shinikizo kumtaka Rais Ruto ajiuzulu

01:29

This browser does not support the video element.

Lakini sheria hiyo ilijumuisha kodi nyingi mpya au zilizoongezwa kwa bidhaa za msingi kama vile mafuta na chakula na miamala ya pesa kwa njia ya simu, pamoja na ushuru wenye utata kwa walipa kodi wote ili kufadhili mpango wa ujenzi wa nyumba.

Sheria hiyo ilisababisha maandamano ya miezi kadhaa yaliyoitishwa na kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga ambayo yaligubikwa na vitendo vya uporaji na makabiliano makali na polisi, na kuibua wasiwasi kuhusu uthabiti wa nchi hiyo kubwa kiuchumi ya Afrika Mashariki.

Soma: Ruto asema maandamano ya Kenya lazima yakome

Muswada mwingine wa fedha wa mwaka huu na vifungu vyake vya nyongeza zaidi ya kodi ili kukusanya mapato mengine ya dola bilioni 2.7, nao pia ulizua wimbi kama hilo la maandamano, lakini wakati huu yakiongozwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Gen-Z wa Kenya.

Jeshi la polisi Kenya lapiga marufuku maandamano NairobiAkikabiliana na mzozo mbaya zaidi wa utawala wake wa takriban miaka miwili, Ruto alitupilia mbali muswada huo ambao tayari ulikuwa umepitishwa na bunge, siku chache baada ya maandamano ya umwagaji damu jijini Nairobi mwezi Juni mwaka huu ambapo waandamanaji walivamia bunge na polisi kuwafyatulia risasi.

Waandamanaji wa Kenya wakipinga muswada wa fedha wa 2024Picha: James Wakibia/ZUMA PRESS/picture alliance

Watu kadhaa wameuawa tangu maandamano hayo yaanze wiki sita zilizopita, huku polisi wakishutumiwa na makundi ya kutetea haki za binadamu kwa kutumia nguvu kupita kiasi. Uamuzi wa mahakama ya rufaa sasa unazua maswali kuhusu uwezo wa serikali kukusanya mapato kutokana na ushuru na kuhudumia deni lake la umma la dola bilioni 78.

Mbali na kusitisha mapendekezo ya nyongeza ya ushuru, Ruto ameanza msururu wa hatua za kujaribu kuwatuliza waandamanaji, ikiwa ni pamoja na kufukuza karibu baraza lake lote la mawaziri.

Wiki iliyopita aliwateua vinara wanne wa upinzani walio karibu na Odinga kujiunga na serikali aliyoitaja kuwa "pana" lakini wanaharakati wanapanga maandamano zaidi mwezi Agosti kumtaka Ruto ajiuzulu.