Mahakama Kenya yailaumu IEBC kwa kuvurunda uchaguzi
20 Septemba 2017Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu ameelezea "ufichuzi wa kustajaabisha" kuhusu mwenendo wa IEBC na kuikosoa makhususi kwa kupuuza agizo la Mahakama ya Juu kuitaka ifunguwe mifumo yake ya kompyuta baada ya upinzani kudai kuwepo na udukuzi.
"Agizo letu na ukaguzi lilikuwa fursa adhimu kwa IEBC kufikisha mahakamani ushahidi kupinga madai ya walalamikaji," Mwilu alisema wakati akisoma ripoti kamili ya hukumu hiyo siku ya Jumatano.
"Ikiwa IEBC haikuwa na chochote cha kuficha, ingetoa ruhusa mara moja ya kuingia katika mifumo yake ya teknolojia ya mawasiliano ili kuonesha kuwa madai ya mlalamikaji hayana msingi. Lakini IEBC ilifanya nini? Ilikaidi maagizo ya mahakama katika maeneo hayo nyeti."
Mawakili wa muungano wa vyama vya upinzani (NASA) unaoongozwa na Raila Odinga, mwezi uliopita walikwenda mahakamani kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta, wakidai kuwepo na wizi, udukuzi na uchakachuaji wa matokeo.
Mfumo wa mawasiliano uliingiliwa
Jaji Mkuu David Maraga aliutangaza uchaguzi wa rais na ushindi wa Kenyatta kuwa batili, katika hukumu aliyoitoa Septemba 1. Mwilu alisema kuwa kufuatia kukataa kwa IEBC kutii maagizo ya mahakama, majaji hawakuwa na budi ila kuamua kwamba "mfumo wa teknolojia ya mawasiliano wa tume hiyo ya uchaguzi uliingiliwa na kudukuliwa, na kwamba data za mfumo huo zilichezewa, au maafisa wa IEBC wenyewe waliingilia data hizo, au walivuruga mfumo wa urushaji matokeo na hawakuwa na uwezo wa kuhakiki data hizo."
Tume ya uchaguzi inatazamiwa kuandaa uchaguzi mpya wa rais kati ya Kenyatta na Odinga Oktoba 17, lakini uamuzi kamili wa Jumatano, pamoja na madai ya upinzani kutaka kuifanyia mageuzi Tume ya Uchaguzi, vimeubua hofu kwamba itakuwa haiwezekani kuitisha uchaguzi katika tarehe hiyo.
Wasiwasi umetawala katika jiji la Nairobi wiki hii kuelekea hukumu hiyo, ambapo polisi imetumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, na ubalozi wa Marekani ukihimiza utulivu. Idara ya mahakama pia imeripoti kupokea vitisho na kulituhumu jeshi la polisi kwa kutotoa ulinzi wa kutosha, madai ambayo polisi imeyakanusha.
Vitisho kwa majaji vyaongezeka
Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rigths Watch limeitaka polisi kuwalinda majaji walioshiriki katika kesi hiyo. Katika matamshi ya wazi siku ya Jumatano, Jaji Mkuu Maraga alitangaza kuwa mmoja wa majaji wanne waliopiga kura kufuta matokeo ya uchaguzi alisafiri nje ya nchi na asingekuwepo mahakamani.
Rais Kenyatta amewaita majaji wa mahakama kuwa "wahuni" na kuonya juu ya hatua ambazo hakuzitaja dhidi ya idara ya mahakama ikiwa atachaguliwa tena mwezi ujao. Wafuasi wa Kenyatta waliandamana nje ya mahakama siku ya Jumanne, kabla ya kutolewa hukumu kamili siku ya Jumatano.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape,rtre,dpae
Mhariri: Mohammed Khelef