1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kenya yawapiga faini waziri, mkuu wa polisi

29 Machi 2018

Mahakam nchini Kenya imewapiga faini waziri wa mambo wa mambo ya ndani Fred Matiang'i na mkuu wa jeshi la polisi Joseph Boinnet baada ya wawili hao kudharau amri yake kuhusu kumuachia mwanasiasa wa upinzani Miguna Miguna

Fred Matiangi vorne links
Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i (kushoto) ametozwa faini ya shilingi laki mbili kwa kudharau mahakama.Picha: Imago/Xinhua Afrika

Waziri wa mambo ya ndani wa Kenya na Inspekta Janerali Mkuu wa Polisi wamepigwa faini kwa kuidharau mahakam siku ya Alhamisi, kwa kushindwa kutii agizo la jaji kumuachia mwanasiasa wa upinzani, katika hukumu iliochochea zaidi mgogoro kati ya mihimili miwili ya dola.

Jaji wa mahakama Kuu George Odunga amesema maafisa hao wawili waandamizi serikalini "walidhihirsha tabia isiyotarajiwa katika zama hizi za kikatiba," - katika ukaripiaji usiokifani kwa maafisa wa juu serikalini.

Waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i, na inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi Joseph Boinet wametozwa kila mmoja shilingi za Kenya 200,000, sawa na dola za Marekani 1,985, kutokana na ushiriki wao katika kumzuwia mwansiasa wa upinzani Miguna Miguna wiki hii.

Mahakama nchini Kenya imekuwa katika msuguano na mhimili wa utawala tangu ilipobatilisha ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi wa Agosti 2017.Picha: Reuters

Miguna Miguna, mwanasiasa maarufu lakini asiechaguliwa kutoka muungano wa upinzani wa NASA, alijipatia umaarufu baada ya kufukuzwa nchini mwezi uliopita, na jaribio lake la kurejea Kenya wiki hii limeshuhudia nchi hiyo ikiingia katika sarakasi za kisiasa.

Wakati Miguna alipozuwiwa kwenye uwanja wa ndege kuhusiana na mgogoro wa uhamiaji, mahakama kuu iliwaamuru mara mbili, waziri wa mambo ya ndani Fred Matiang'i, mkuu wa jeshi la polisi Joseph Boinnet na kamishna mkuu wa idara ya uhamiaji kumfikisha mahakamani.

Mvutano kati ya mihimili mikuu miwili

Vita vinavyozidi kati ya serikali na mahakama - tangu mahakama ya juu kabisaa ilipobatilisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta mwaka uliopita -- vimeshuhudia maafisa wa serikali wakipuuza amri kadhaa za mahakama.

Kufukuzwa kwa kwanza kwa Miguna kulikuja baada ya kukamatwa kwa tuhuma za uhaini kutokana na kushiriki kwake katika tukio la kujiapisha kwa Raila Odinga, aliesisitza kuwa yeye ndiye alikuwa mshindi halali wa uchaguzi wa mwaka uliopita.

Wizara ya mambo ya ndani ya Kenya inasema Miguna alipoteza uraia wake kwa kuchukuwa uraia wa Canada miaka kadhaa iliopita -- wakati ambapo uraia wa nchi mbili ulikuwa hauruhusiwi.

Mwezi Februari, mahakama iliiamuru serikali kumruhusu Miguna arejee, na kumpatia hati mpya ya kusafiria au imruhusu aingie nchini kwa kutumia hati yake ya Canada, wakati akisubiri kusikisiliza shauri la kutetea uraia wake wa Kenya.

Hata hivyo, Miguna alipowasili siku ya Jumatatu, alikataa kuomba visa ya miezi sita, kuingia kwa kutumia hati yake ya Canada au kujaza fomu za kuhalalisha uraia wake.

Miguna Miguna (kulia mwenye kofia) akihudhuria tukio la kujiapisha kwa RailaOdinga Januari 30, 2018.Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

"Alikataa kusaini nyaraka za kuingia nchini na kuzichana. Alisalia hapa kwa siku mbili na kila zilipopelekwa kwake alitukaripia kwamba yeye ni Mkenya," alisema afisa uhamiaji kwa sharti la kutotajwa jina.

Polisi wamalizia hasira kwa waandishi

Siku ya Jumatatu, polisi wa uwanja wa ndege waliwashambulia na kuwajeruhi waandishi kadhaa wa habari waliokuwa wanaripoti sakata hilo katika tukio lililorekodiwa na kulaaniwa na kamati ya kuwalinda waandishi habari.

Katika taarifa kutoka Dubai, Miguna alisema alizuwiwa chooni kwa siku mbili katika uwanja mkuu wa ndege wa Kenya, na kudai kuwa maafisa walimuangusha chini na kumpiga sindano yenye vitu visivyoeleweka na kumsababishia kupoteza fahamu.

Tukio hilo limekuja wiki kadhaa baada ya maridhiano ya kushtukiua kati ya Odinga na Kenyatta kufuatia msimu wa mgumu wa uchaguzi. Karibu watu 100 waliuawa, wengi wao na jeshi la polisi, wakati wa machafuko ya uchaguzi, kulingana na mashirika ya haki za binadamu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe.

Mhariri: Saumu Yusuf