Mahakama Kuu Kenya: Hatuna uwezo kesi ya Kenyatta, Rutto
15 Februari 2013
Mahakama kuu ya Kenya imesema haina uwezo kisheria kuamua kama wagombea urais katika uchaguzi ujao nchini humo, Uhuru Kenyatta na mgombea wake mwenza William Ruto, waendelee kugombea au la.
Matangazo
Jopo la majaji watano wa mahakama hiyo, wamesema muda mfupi uliopita kuwa mahakama hiyo haina uwezo wa kushughulikia suala linalohusu kugombea urais, wakisema ni mahakama ya juu kabisa pekee ambayo inao uwezo huo.
Viongozi hao wa Muungano wa Jubilee wamepata afueni sasa baada ya Mahakama Kuu sasa kuhamishia kesi hiyo kwenye Mahakama ya Juu.
Mahakama hiyo imesema kwa kuwa tayari Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeshakubali uteuzi wa Kenyatta na Rutto kushiriki kwenye uchaguzi mkuu ujao, mahakama hiyo haina mamlaka ya kubadilisha uamuzi wa IEBC.
Mahakama hiyo imesma kwamba inao tu uwezo wa kuchunguza upya uamuzi wa IEBC kuhusu wagombea wengine lakini si wagombea urais na wagombea wenza wao.
Uamuzi wa Mahakama Kuu
Akiotoa uamuzi huo Jaji Msagha Mbogoli: “Taasisi ambayo ingekuwa na uwezo wa kikatiba wa kuamua kesi hiyo ni IEBC chini ya kifungu nambari 88 4 (e) cha Katiba ambacho na sehemu ya 74 ya sheria za uchaguzi ambacho kinatoa ruhusa kwa Tume ya Uchaguzi kutoa uamuzi juu ya kesi kama hiyo. Hivyo basi, ingekuwa tofauti ikiwa Tume ya IEBC ingeshindwa kutekeleza wajibu wake.”
Mahakama hiyo imesema kwamba wawili hao hawana hatia hadi watakapohukumiwa katika kesi yao inayowakabili huko The Hague na hakuna mtu anayeweza kubashiri iwapo wawili hao watapatikana na hatia.
Kesi hiyo ilifunguliwa na vyama vya kiraia vikipinga ushiriki wa wawili hao katika uchaguzi wa hapo tarehe 4 Machi, kwa madai kuwa wamekosa uadilifu kwa sababu wagombea hao tayari wamefunguliwa mashtaka ya kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).
Mahakama hiyo imesema kwamba endapo mahakama ya ICCingewasimamisha wawili hao kugombea nyadhifa za uongozi, basi hilo lingeliwezekana. Mahakama hiyo imeamua gharama ya washtakiwa kwenye kesi hiyo ilipwe na wenye kushtaki.
Mwandishi: Alfred Kiti/DW Nairobi Mhariri: Mohammed Khelef