1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kuu Kenya yasimamisha mchakato wa kumtoa Gachagua

18 Oktoba 2024

Mahakama Kuu nchini Kenya imeusimamisha kwa muda mchakato wa kumteua naibu mpya wa rais baada ya kupokea kesi ya pingamizi ya naibu wa rais aliyefutwa kazi.

Jaji wa Korti Kuu ya Kenya Chacha Mwita
Jaji wa Korti Kuu ya Kenya Chacha Mwita Picha: Shisia Wasilwa/DW

Spika wa bunge la taifa nchini Kenya amelichapisha rasmi jina la naibu wa rais mteule Kithure Kindiki kwenye gazeti rasmi la serikali. Wakati huohuo, mahakama kuu imesitisha kwa muda kuondolewa kwa Rigathi Gachagua kwenye nafasi yake ya unaibu raisi na uteuzi wa mrithi wake hadi Oktoba 24. Rigathi Gachagua aliyelazwa hospitalini baada ya kupata maumivu makali ya kifua alitimuliwa Alhamisi usiku na baraza la Senate kwa mashtaka ya uongozi mbaya na ufisadi.

Mkwamo wa kikatiba wazuka

Uamuzi wa mahakama kuu ya Kenya wa kusitisha kwa muda uamuzi wa Senate wa kumuondowa madarakani Rigathi Gachagua kuwa naibu rais, umeivuruga mipango ya serikali ya kumuapisha rasmi mrithi wake mpya.Jaji Richard Mwita kadhalika amesitisha uteuzi wa mrithi wa Gachagua hadi tarehe 24 mwezi huu wa Oktoba.

Kwa sasa Jaji Mkuu Martha Koome anatazamiwa kuteua jopo la majaji watakaosikiliza na kuamua hoja za kikatiba zilizoibuliwa na kambi ya Rigathi Gachagua. Kwa kufuata taratibu za dharura, wakili mkongwe Paul Muite anashikilia kuwa mashtaka yaliyomsulubisha Rigathi Gachagua mbele ya bunge la Taifa na baraza la Senate hayana mashiko.

Kwa mujibu wa wakili Paul Muite, baraza la Senate lilitakiwa kutoegemea upande wowote lilipokuwa linatathmini mashtaka hayo ya ufisadi na kukiuka katiba na hivyo ushahidi uliotolewa ulikuwa na walakini.

Mashtaka 5 kati 11 yalimhukumu Gachagua

Baraza la Seneti na Bunge lamtia hatiani GachaguaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Mbali na mashtaka ya kujilimbikia mali kwa njia zisizokuwa sawa, rais Gachagua alituhumiwa kwa kutumia watu wa kando kujipatia kandarasi ya vyandarua vya mbu vilivyotiwa dawa vya thamani ya shilingi bilioni 3.7 kupitia mamlaka ya ununuzi wa bidhaa za tiba, KEMSA.

Kulingana na mswada huo,naibu wa rais aliwashinikiza viongozi wa KEMSA kumpa kandarasi hiyo ya vyandarua vya mbu kutumia kampuni ya Crystal Ltd kinyume na utaratibu.

Hoja nyengine iliyoibuka ni kuwa naibu wa rais amekuwa akitoa kauli zinazoashiria kuwa wakenya wananufaika kwa kuzingatia mchango wao wa kisiasa kupitia vyama jambo ambalo limewakirihi wengi. Mashataka hayo pia yalijikita katika suala la naibu wa rais kujilimbikia mali kama vile hoteli ya kifahari ya Outspan,Olive Gardens na Treetops kwa kasi , hali inayoashiria kuwa kuna mkono wa ufisadi

Kusubiria hatima ya kesi au amri itupiliwe mbali

Mfahamu Kithure Kindiki mrithi wa Gachagua

02:17

This browser does not support the video element.

Kimsingi serikali sasa inaweza kusitisha mipango hiyo hadi kesi iliyowasilishwa kuamuliwa au ifike mahakamani ili amri hiyo ya kusitisha uteuzi na kumuapisha mrithi wa Gachagua kufutiliwa mbali.

Duru zinaeleza kuwa mipango ilidhamiria kumuapisha Kithure Kindiki kuwa naibu wa rais kwenye uga wa Kasarani au jumba la mikutano la KICC Jumamosi kesho asubuhi ili aweze kuhudhuria maadhimisho ya siku ya mashujaa ya mwaka huu yalipangwa kufanyika Jumapili katika kaunti ya Kwale.Wakenya wana mtazamo upi kuhusu mchakato mzima wa kumuondoa Rigathi Gachagua madarakani? Geoffrey Kokoyo mkaazi wa Baringo anashikilia kuwa, "Ruto hakutufafanulia makosa aliyoyafanya Rigathi Gachagua.Tumeambiwa tu alijilimbikizia mali na mambo mengine mengi yasiyokuwa na ushahidi.Inakuwa vigumu kuamini mchakato huo.", anaelezea Kokoyo. 

Naibu rais lazima aapishwe na Jaji Mkuu

Naibu wa Rais Mteule KIthure KindikiPicha: James Kamau Wakibia/Anadolu/picture alliance

Ifahamike kuwa shughuli ya kumuapisha rasmi naibu wa rais sharti isimamiwe na idara ya mahakama.Kisheria, Jaji Mkuu Martha Koome ndiye anayewajibika kumuapisha naibu wa rais inaeleza ibara ya 148 ya katiba ya Kenya.

Mapema wakati wa mchana,Spika wa bunge la taifa Moses Wetangula alilichapisha jina la Kithure Kindiki kwenye gazeti rasmi la serikali kuwa naibu wa rais mteule.Bunge la taifa lilipokea taarifa ya Rais William Ruto ya kumteua waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki kuwa naibu wake badaa ya baraza la Senate kupiga kura kumbandua usiku wa kuamkia leo. Sammy Rotich kutokea Baringo anaamini ni kuwa, "Ni sawa kabisa kwa Kindiki kuwa pale kwani ni mchapa kazi, msomi na anaelewa wakenya kwani amekuwa waziri wa usalama wa taifa.Hatima ya Kenya iko vizuri. Nimefurahi sana.", anasimulia Rotich.

Hayo yalijiri baada ya wabunge 236 kupiga kura kumuidhinisha Kithure Kindiki kuwa naibu wa rais kwenye kikao maalum. Hakuna mbunge aliyepinga au kususia uteuzi huo.Wakaazi wa Tharaka Nithi anakotokea naibu wa rais mteule Kithure Kindiki wamepokeaji hatua hii? Mary Muthoni anaamini kuwa, "Kindiki akishikana na Ruto tutaenda mbali.Hii ni kwasababu sasa sauti ya wanyonge imesikika kwani mtu wa kutokea kabila dogo amepewa nafasi kungoza afisi kubwa ya taifa.", anaelezea.

Kindiki apongezwa na wafuasi wake

Bunge la taifa lilipokea taarifa ya Rais William Ruto ya kumteua waziri wa usalama wa taifa Kithure Kindiki kuwa naibu wake badaa ya baraza la Seneti kupiga kura kumbandua usiku wa kuamkia leo. Wakaazi wa kijiji cha Irunduni anakotokea Kithure Kindiki walisherehekea na kuimba nyimbo ya taifa.

Kindiki aliwahi kuwa seneta wa kaunti ya Tharaka Nithi kwa mihula miwili na alikuwa mmoja ya waliotazamiwa kuwa mgombea mwenza wa William Ruto wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita wa 2022.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW