1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Sheria na HakiKenya

Mahakama kuu Kenya yazuia kupelekwa vikosi vya usalama Haiti

Hawa Bihoga
9 Oktoba 2023

Mahakama kuu ya Kenya imezuia kwa muda kupelekwa kwa vikosi vya usalama vya nchi hiyo katika mataifa mengine kwa muda wa wiki mbili hadi kesi ya msingi iliowasilishwa na mwanansia nchini humo itaposikilizwa.

Jaji mkuu wa mahakama kuu Martha Koome
Jaji mkuu wa mahakama kuu Martha KoomePicha: John Ochieng/SOPA Images/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Hatua hii ni baada ya Kenya kukubali kuongoza kikosi cha mataifa mbalimbali kukabiliana na ghasia za magenge ya uhalifu nchini Haiti kufuatia azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililoidhinishwa wiki iliopita.

Marekani iliahidi kutoka kiasi cha hadi dola milioni 200 kufanikisha operesheni ya ujumbe huo, huku mataifa mengine yakitoa ahadi ya ufadhili pia.

Aliyekuwa mgombea urais, Ekuru Aukot, aliwasilisha ombi siku ya Ijumaa dhidi ya kupelekwa kwa vikosi va Kenya- nchini Haiti, akisema kuwa sheria ya kumruhusu rais kufanya hivyo ni kinyume na vifungu vya katiba.

Soma pia:Rais wa Kenya William Ruto apongeza azimio la Baraza la Usalama la UN kuhusu Haiti

Ombi la mwanasiasa huyo pia lilimkosoa Rais William Ruto kwa kukubali kuongoza ujumbe wa kimataifa ya kulinda amani huku Kenya ikihangaika na masuala ya usalama yanayotokana na mashambulizi ya wanamgambo na hivi karibuni ikishuhudia mapigano ya kikabila.

Jaji wa Mahakama Kuu, Chacha Mwita, siku ya Jumatatu, alitoa siku tatu kwa waliolalamikiwa katika shauri hilo akiwemo Rais Willium Ruto, waziri wa mambo ya ndani na Mkuu wa Jeshi la polisi, kutoka majibu ya kisheriakwa Aukot. Shauri hilo limehairishwa hadi Oktoba 24.

Mpango huo wakosolewa Kenya

Wiki iliyopita, kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, alikosoa ushiriki wa Kenya katika ujumbe wa kulinda amani wa Haiti, akisema nchi ilikuwa na changamoto zake za kiusalama.

Askari jeshi Kenya wakiwa katika majukumu yao ya kulinda usalama Picha: John Ochieng/SOPA/ZUMA/picture alliance

Kenya ilikuwa bado haijathibitisha tarehe ya kupelekwa kwa maafisa hao 1,000 iliopanga kupeleka Haiti.

Soma pia:Jeshi la polisi nchini Haiti limeelemewa na wingi wa magenge na uhalifu unaofanywa na magenge hayo

Rais Willium Ruto alisema mnamo Oktoba 3 kwamba kikosi kinachoongozwa na Kenya "hakitawaangusha watu wa Haiti."

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa kuanzia Januari 1 hadi Agosti 15, zaidi ya watu 2,400 nchini Haiti waliripotiwa kuuawa, wengine zaidi ya 950 wakitekwa nyara na wengine 902 kujeruhiwa.

Magenge ya wahalifu yawahangaisha raia Haiti

02:09

This browser does not support the video element.