1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama Kuu Tanzania yatupilia mbali mapingamizi ya Lissu

22 Septemba 2025

Mahakama Kuu nchini Tanzania imetupilia mbali mapingamizi yaliyotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu kuhusu makosa aliyoyabaini katika hati ya mashitaka na hitilafu katika viambatanisho vya hati ya mashitaka.

Tanzania | Tundu Lissu
Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA Tundu LissuPicha: Ericky Boniphase/DW

Amegonga mwamba tena. Hivyo ndivyo tunavyoweza kusema baada ya mahakama kuu masijala ndogo ya Dar es Salaam, kuyatupilia mbali mapingamizi yaliyowekwa na Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, katika kesi ya uhaini inayomkabili.

Mara baada ya kesi hiyo kupelekwa Mahakama Kuu na kisha mwanasiasa huyo kusomewa mashitaka, alibainisha mapungufu katika maeneo ya kesi hiyo ikiwamo kukosewa kwa hati ya mashitaka, hitiflafu katika viambatanisho vya hati ya mashitaka, mamlaka ya mahakama kuu na kesi hiyo  na utata katika maelezo ya mashahidi.

Hata hivyo baada ya mapingamizi mawili ya awali kugonga mwamba, mahakama imeyatupilia mbali mapingamizi yaliyotolewa na Lissu, la kwanza hitilafu katika hati ya mashitaka na  la pili ni hoja ya Lissu kuwa viambatanisho vya hati ya mashitaka vipo kinyume na sheria.

Pamoja na hayo, Mahakama imeikataa hoja ya Lissu kutaka kesi hiyo iendeshwe katika mahakama ya wazi ikiwamo kurusha kesi hiyo mubashara ambapo Mahakama imeamua kuwa tayari mahakama hiyo ni ya wazi lakini kwa kuwa kuna mashahidi wanaopaswa kulindwa, mwenendo wa kesi hauwezi kurushwa mubashara.

Baada ya uamuzi huo, mahakama iliendelea kwa upande wa Jamhuri kusoma maelezo ya awali ya kesi hiyo na jaji alimsomea mashitaka yake.

Wakili kiongozi wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala amezungumzia uamuzi huo wa Mahakama.

"Tunaheshimu uamuzi wa mahakama lakini hatukubaliani kwa sababu tunaamini kuwa kuna upungufu mkubwa ambao upo wazi, lakini tunaamini kuwa uamuzi huo haumui kesi moja kwa moja, inabidi Kwenda nao hivyo hivyo”

Nae Wakili wa Kujitegemea,  William Kahale anasema taifa linapoelekea katika uchaguzi hali inaweza kutasiriwa tofauti.

"Maamuzi ya mahakama yataendelea kuheshimiwa, lakini sasa kwa upande huu wa mtizamo wa kisiasa, kwamba kuna uchaguzi unaendelea nchini Tanzania na mpinzani mkuu kwenye uchaguzi huu ambaye  labda anaogopwa, labda anaweza kutoa upinzani kwenye chama kilichopo madarakani ndio huyu anayeshitakiwa katika hii kesi, ndiye huyo anayeshitakiwa kwa kosa la uhaini  ambalo ni kosa kubwa zaidi,  kwa hiyo inatoa picha tofauti kidogo”

Baada ya hoja za awali kusikilizwa na Lissu kujibu kila hoja akiyakanusha mashitaka aliyoseomewa, sasa kesi itapangiwa kusikilizwa ikiwamo mashahidi kuletwa mahakamani.

Lissu alikamatwa Aprili 4 mwaka huu akiwa wilaya ya Mbinga , mkoa wa Ruvuma katika mkutano wa kisiasa wa Chadema, na baadaye kushitakiwa kwa makosa ya uhaini. Kesi hiyo imepelekwa mbele mpaka Oktoba sita.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW