1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama kyamlaza tena Mbowe rumande

Hawa Bihoga29 Novemba 2018

Mahakama Kuu ya Tanzania hapa jijini Dar es Salaam, imesikiliza rufaa ya dharura ya Mbowe na mwezie Matiko dhidi ya Jamhuri baada ya kukwama hasiku ya Jumatano kutokana na nyaraka muhimu kukosekana.

Anführer von Tansanias Oppositions-Partei Chadema
Picha: DW/E. Boniphace

Mahakama mkuu nchini Tanzania imesema kuwa itatoa hukumu ya rufaa ya dharura inayomkabili mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Chadema na mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Freeman Mbnowe, pamoja na mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, baada ya kusikilizwa kwa pande zote mbili. Mbowe na Matiko walifutiwa dhamana mnamo Novemba 23 baada ya kutajwa kukiuka masharti ya dhamana katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Mahakama Kuu ya Tanzania hapa jijini Dar es Salaam, imesikiliza rufaa ya dharura ya Mbowe na mwezie Matiko dhidi ya Jamhuri baada ya kukwama hapo jana kutokana na nyaraka muhimu kukosekana. Mawakili wa pande zote mbili walifika mahakamani wakiwa na nyaraka ambazo walizihitaji kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa kesi hiyo:

Upande wa Jamhuri umeiambia mahakama kuwa maombi ya rufaa yana kasoro kutokana na vifungu vya sheria vilivyotumika katika kuyaandaa kutokuwa sahihi, kwa kunukuu kifungu cha sheria nambari 261 kinachoeleza uhalali wa rufaa inayotolewa mahakamani ili ikubalike ndani ya siku kumi.

Vifungu vya sheria nambari 359 katika kifungu kidogo cha kwanza na sheria nambari 362, vinadaiwa kutumika kwa rufaa hiyo ambapo upande wa mashtaka umedai vifungu hivyo havijatumika ipasavyo katika uwasilishwaji wa rufaa hiyo.

Picha: DW/B. Riegert

Lakini pia hoja ya nyaraka ambazo zilileta mkwamo wa usikilizwaji wa shauri hilo hapo jana nayo ilizingatiwa na upande wa mashtaka kuwa nyaraka zilizowafikia hazikuwa tayari kutokana na kuandikwa kwa mkono hivyo hazisomeki vyema na kutumia kifungu cha 13 ibara ya 6a cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inachoelekeza kila mmoja ana haki ya kusikilizwa hivyo udharura uliotumika haukufuata utaratibu.

Upande wa utetezi ukiwa na jopo la mawakili saba wakiongozwa na Peter Kibatala umeiambia mahakama kuwa hoja hizo hazina msingi kwa kuwa nyaraka zilizotumika kufuta dhamana ziliandaliwa na upande wa mashtaka, hivyo kuiomba mahakama itengue maamuzi ya kufutiwa dhamana kwa wateja wao na kuongeza kuwa rufaa iliyopo mbele ya Jaji Sam Rumanyika ni halali na inalindwa kwa misingi ya sheria na katiba.

Baada ya kusikilizwa kwa pande zote mbili kwa muda wa takriban masaa matatu, Jaji Rumanyika akaiambia mahakama kuwa atatoa uwamuzi wake hapo kesho majira ya saa tano asubuhi. Nje ya mahakama wafuasi wa chama hicho waliimba nyimbo za chama na mshikamano. 

Mwandishi: Hawa Bihoga/DW Dar es Salaam

Mahriri: Mohammed Khelef

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW