Mahakama Misri yaidhinisha kifungo cha mwanasiasa maarufu
28 Mei 2024Mgombea wa zamani wa urais Ahmed Altantawy aliwekwa kizuizini na vikosi vya usalama katika mahakama hiyo mjini Cairo baada ya uamuzi huo. Wakili wake Khaled Ali ameyasema hayo.
Altantawy alipatikana na hatia na kuhukumiwa Februari 2024 pamoja na wasaidizi wake 22, akiwemo msimamizi wa kampeni zake, kwa mashitaka ya kusambaza fomu zisizoruhusiwa za kuidhinisha kugombea kwake.
Mahakama hiyo pia ilimzuia Altantawy kushiriki uchaguzi wa kitaifa kwa miaka mitano ijayo. Mwanasiasa huyo alikuwa ameachiwa kwa dhamana wakati wa kesi hiyo ya rufaa.
Altantawy, ambaye alionekana na wengi kuwa mgombea halisi wa upinzani, alijiondoa katika mbio za urais mwaka jana baada ya kushindwa kupata idadi ya sahihi kutoka kwa wapiga kura inayohitajika ili kupewa uteuzi.
Sissi alishinda karibu asilimia 90 ya kura, kwa mujibu wa Tume ya Kitaifa ya Uchaguzi nchini Misri. Alishinda muhula wa tatu madarakani ambao utakamilika mwaka wa 2030.