1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Mahakama Pakistan yamtia hatiani Waziri Mkuu wa zamani

10 Mei 2023

Mahakama ya Pakistan mjini Islamabad imemtia hatiani waziri mkuu wa zamani Imran Khan katika tuhuma za kuuza zawadi za serikali wakati wa utawala wake wa miaka minne.

Pakistan | Imran Khan | ehemaliger Premierminister
Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan Imran KhanPicha: Akhtar Soomro/REUTERS

Uamuzi huu wa mahakama umetolewa leo mchana baada ya kukamatwa hapo jana kwa kiongozi huyo. 

Mahakama ya Islamabad imeamua kwamba waziri mkuu wa zamani Imran Khan anaweza kushikiliwa kwa siku nane zaidi, huo ukiwa ni uamuzi uliotolewa baada ya mwanasiasa huyo kufikishwa mahakamani hii leo kufuatia kukamatwa kwake jana jumanne.

Mahakama ya kupambana na rushwa imemtia hatiani kwa kuhusika na wizi wa zawadi za serikali na kisha kuziuza.

Soma pia: Mamia waandamana kukamatwa kwa Imran Khan wa Pakistan

Hali ni ya mashaka makubwa nchini humo huku polisi wakiwa wametawanywa kila kona ya nchi na katika mji wa Islamabad  polisi wameweka makontena makubwa  kwenye barabara zinazoelekea ofisi za polisi anakoshikiliwa  Imran Khan.

Kukamatwa kwa Imran Khan kulizusha vurugu kubwa jana yakizuka mapambano katika miji mbali mbali kati ya polisi na wafuasi wa mwanasiasa huyo aliyewahi kuwa mcheza kriketi na takriban watu sita waliuwawa.

Vurugu zazuka kati ya wafuasi wa Imran Khan na polisi

Wafuasi wa Imran Khan wakikabiliana na polisi nje ya majengo ya mahakama mjini Islamabad.Picha: Akhtar Soomro/REUTERS

Kuendelea kushikiliwa kwake na polisi kumeongeza uwezekano wa kuzuka vurugu zaidi. Tayari waandamanaji wenye hasira wameshavamia kituo kimoja cha redio huko Kaskazini Magharibi hivi leo na wafuasi wake wakiripotiwa kukabiliana na polisi mjini Islamabad.

Waziri wa mipango nchini humo Ahsan Iqbal ameitaja hasara iliyosababishwa na vurugu nchini humo, "Uharibifu uliosababishwa kwenye  miundo mbinu ya serikali na vitu ni wa  mabilioni. Unajuwa wameharibu magari ya polisi, mabasi, kituo cha mabasi ya metro na shule nyingi. Kwa hivyo hii ni hasara kwa walipa kodi. Ni hasara kwa watu masikini wa Pakistan''

Chama cha Imran Khan, Tehreek-e-Insaf kimetowa mwito wa utulivu ingawa mvutano huu unaiweka nchi hiyo kwenye hali kubwa ya tahadhari baada ya machafuko ya jana.

Soma pia: Wanajeshi 4 wa Pakistan wauawa katika shambulio la mpakani

Kutiwa hatiani waziri mkuu huyo wa zamani kumefuatia uamuzi  uliotolewa na tume ya uchaguzi mwezi Oktoba, iliyomkuta na hatia ya kuuza kinyume cha sheria zawadi za serikali kati ya mwaka 2018 na mwaka 2022 na kumzuia kushikilia nafasi yoyote ya ofisi ya umma hadi utakapofanyika uchaguzi ujao mwezi Novemba.

Imran Khan mwenyewe amekanusha kuhusika na makosa yoyote.

Polisi wa kupambana na ghasia wakimkamata mfuasi wa waziri mkuu wa zamani Imran Khan.Picha: ARIF ALI/AFP

Waziri wa mipango Ahsan Iqbal kama mtendaji serikalini ameshikilia kwamba sheria ichukue mkondo wake, "Bwana Imran Khan atakabiliwa na sheria.Ikiwa atakutwa hana hatia atashiriki uchaguzi lakini ikiwa atakutwa na hatia ya ufisadi bila shaka atabidi akabiliwe na hatua za kuhusika na ufisadi huo''

Gazeti la Dawn la nchini humo katika makala yake iliyochapishwa leo limesema ukubwa wa maandano ya jana na namna yalivyozuka baada ya kukamatwa kiongozi huyo inatowa ishara kwamba hasira za umma zinaelekezwa pia kwa jeshi.

Mara kadhaa Imran Khan amesikika akiwatuhumu maafisa waandamizi jeshini kwamba wanapanga njama za kutaka kumuua.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW