1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wafanyakazi wa 'Cumhuriyet' wakamatwa

5 Novemba 2016

Waandishi wa habari tisa wa gazeti la upinzani nchini Uturuki la Cumhuriyet, wamekamatwa kwa tuhuma ya makosa yanayohusiana na ugaidi, kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi yao.

Türkei Cumhuriyet Chefredakteur festgenommen
Picha: Getty Images/AFP/O. Kose

Mahakama Kuu ya mjini Istanbul leo iliamuru kukamatwa na kufungwa waandishi hao wa habari akiwemo mhariri mkuu wa gazeti hilo, Murat Sabuncu, ambaye alikamatwa pamoja na wafanyakazi wengine siku ya Jumatatu. Shirika binafsi la habari, Dogan limesema mchora katuni Musa Kart pamoja na mwandishi wa makala, Kadri Gursel pia wamekamatwa.

Wafanyakazi hao wa Cumhuriyet wanashutumiwa kwa kuwa na mafungamano na wanamgambo wa Kikurdi pamoja na Fethullah Gullen, aliyeko uhamishoni nchini Marekani na ambaye Uturuki inamtuhumu kwa kuhusika na kupanga jaribio la mapinduzi la Julai 15. 

Uamuzi huo wa mahakama umetolewa siku moja baada ya wabunge tisa kutoka chama cha upinzani cha Kurdish People's Democratic-HDP, kinachowaunga mkono Wakurdi, kukamatwa kutokana na aina ya makosa yanayohusiana na ugaidi, hatua iliyokosolewa vikali na Umoja wa Ulaya pamoja na mashirika ya haki za binaadamu. Miongoni mwa wabunge waliokamatwa ni pamoja na viongozi wenza wa chama hicho Selahattin Demirtas na Figen Yuksekdag.

Polisi wakiwalinda wafuasi wa HDP nje ya mahakama ya IstanbulPicha: Reuters/S. Kayar

Hata hivyo, gazeti la Cumhuriyet ambalo limeendelea kuchapisha taarifa zake wiki hii licha ya kamatakamata hiyo, limekanusha madai yote hayo na pia limethibitisha kuhusu kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa wafanyakazi hao. Marekani pia imeelezea wasiwasi wake kuhusu udhibiti na mipaka ya uhuru wa kujieleza nchini Uturuki.

Wasiwasi kuhusu kukiukwa haki za binaadamu

Mhariri wa zamani wa gazeti hilo, Can Dundar, alifungwa mwaka uliopita kwa kuchapisha siri za serikali zinazohusu jinsi Uturuki ilivyowasaidia kwa silaha wapiganaji wa Syria. Kesi ya Dundar ilizusha lawama kutoka makundi ya kutetea haki za binaadamu na mataifa ya Magharibi yakielezea wasiwasi wao kuhusu hali mbaya ya haki za binaadamu nchini Uturuki, chini ya utawala wa Rais Recep Tayyip Erdogan. Tangu wakati huo, Dundar alikimbilia nchini Ujerumani na anaishi Berlin.

Cumhriyet lilianzishwa mwaka 1924, hivyo kuwa gazeti kongwe zaidi katika jamhuri ya Uturuki, gazeti hilo kwa muda mrefu limekuwa likimkosoa Rais Erdogan pamoja na chama tawala chenye misingi ya Kiislamu cha Haki na Maendeleo AKP, ambacho Erdogan ni mwanzilishi mwenza.

Aliyekuwa mhariri wa Cumhuriyet, Can DundarPicha: picture-alliance/dpa/S. Prautsch

Tangu kushindwa kwa jaribio la mapinduzi, magazeti, majarida, vituo vya televisheni na mashirika ya habari 170 yamefungwa, na kuwaacha waandishi wa habari 2,500 bila ajira. Umoja wa waandishi wa habari nchini Uturuki umesema katika taarifa yake kwamba inapinga hatua ya kuwekwa kizuizini waandishi hao.

Wakosoaji wa serikali wamesema kamatakamata dhidi ya vyama vya upinzani na vyombo vya habari, inatumika kuwanyamazisha wapinzani nchini Uturuki, ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO na nchi ambayo bado inasema ina nia ya kujiunga na Umoja wa Ulaya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/Reuters,DPA,AFP
Mhariri: Mohammed Dahman