Mahakama ya Afrika Mashariki yakataa rufaa ya Tanzania
10 Juni 2020Pamoja na mambo mengine sheria hiyo inatajwa kukiuka mkataba wa Afrika mashariki pamoja na kuminya uhuru wa kupata habari.
Jaji kiongozi katika kesi hiyo Godffrey Kiryabwire ,akitoa hukumu dhidi ya kesi iliyowasilishwa katika mahakama hiyo na baraza la habari Tanzania MCT, mtandao wa watetezi wa haki za binadamu pamoja na kituo cha sheria na haki za binadamu, iliyopinga nia ya serikali ya Tanzana ya kukataa rufaa kupinga maamuzi ya mahakama yaliyowapa ushindi MCT na washirika wake mwaka jana 2019.
Rufaa ya serikali ya Tanzania yakosa kukidhi matakwa ya kisheria
"Mahakama imeamua kuwa nia ya rufaa ya serikali ya Tanzania inatupiliwa mbali kwa sababu ya kutokidhi baadhi ya matakwa ya kisheria.” Jaji Godfrey Kiryabwire amesema hayo kwenye hukumu aliyoitoa mahakamani.
Mwaka 2017, baraza la habari Tanzania pamoja na watetezi wa haki za binadamu walipeleka maombi katika mahakama ya Afrika mashariki kupinga vifungu kadhaa vya sheria ya huduma ya habari ya mwaka 2016 wakidai kuwa vinakinzana na vifungu vya mkataba ulioanzishwa na jumuiya ya Afrika mashariki.
Ushindi kwa MCT
Mahakama hiyo ilitoa ushindi kwa MCT na washirika wake na serikali ya Tanzania ikapeleka ombi la kukata rufaa kupinga maamuzi hayo. Kutokana na mahakama hiyo kutupilia mbali nia ya serikali ya kukata rufaa watetezi wa haki za binadamu wanasema sheria hiyo sasa inatakiwa kufanyiwa marekebisho.
Baraza la habari Tanzania sasa linajipanga kuwaelimisha wanahabari na wadau wa habari kuhusu vipengele 16 vinavyotakiwa kubadilishwa, na wanaimani serikali itatoa ushirikiano kutekeleza maamuzi yalitolewa na mahakama ya Afrika mashariki. Kwa njia ya simu nimemuuliza Kajubi Mkajanga katibu mtendaji wa baraza la habari Tanzania maamuzi hayo ya mahakama yanatoa taswira gani kwa tasnia ya habari Tanzania?
Hukumu hiyo imetolewa kwa njia ya video kutokana na hofu ya maambukizi ya virusi vya Corona.