AfCHPR yatimiza miaka 20 tangu ilipoanza kazi zake Afrika
13 Machi 2026
Hata hivyo miongoni mwa changamoto zinazoikabili mahakama hiyo ni utekelezaji wa maamuzi yake, pamoja na baadhi ya nchi wanachama kutoridhia au kujiondoa katika itifaki inayowaruhusu wananchi wao kupeleka kesi moja kwa moja katika Mahakama hiyo.
Ni katika kipindi ambacho pia Mahakama hiyo imempata Rais mpya aliyechaguliwa na majaji 11 wa Mahakama hiyo inayoshughulikia haki za binadamu, ikiwa ni uchaguzi wa kawaida wa kupokezana miongoni mwa majaji, nafasi inayodumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Rais mpya wa Mahakama ya Afrika ya haki za binadamu na watu kwa sasa ni jaji Braise Tchikaya raia wa Jamhuri ya Kidekokrasia ya Kongo, akichukua nafasi ya jaji Modibo Sako wa nchini Mali. Tchikaya anakabiliwa na kibarua cha kusimamia Haki za binadamu barani Afrika, hasa utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama. Baada ya kuchaguliwa anasisitiza kuwa Mahakama hiyo inanguvu ya kupiga marufuku maamuzi binafsi ya mahakama za ndani.
"Mahakama hii ni jukwaa la juu la kimataifa, maamuzi yote ya Mahakama za ndani za nchi binafsi na majaji 11 wa mahakama hii wananguvu ya kupiga marufuku maamuzi ya mahakama za ndani. Wakati Mahakama ilipoanzishwa baadhi ya maraisi walisema hakuna rasilimali za kutosha, lakini nchi kama Burkina Faso na Senegal zilisisitiza kwamba Mahakama ya Afrika inahitajika.”
Tanzania yatakiwa kurekebisha vifungu vyake vya katiba
Kesi za mwanzo zilizotolewa maamuzi ndani ya mwezi huu wa Machi chini ya Uongozi wa Tchikaya ni kuhusu uchaguzi na demokrasia ya Tanzania, ambapo mahakama hiyo imeipa Tanzania miezi 24 kurekebisha baadhi ya vifungu vyake katiba ya Tanzania bara na visiwani vinavyozuia mahakama za ndani kushughulikia pingamizi za matokeo ya uchaguzi wa urais.
Katiba ya Tanzania, inaruhusu Tume ya Taifa ya uchaguzi NEC na katiba ya Zanzibar inaruhusu Tume ya Taifa ya uchaguzi Zanzibar ZEC kutokuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa matokeo ya uchaguzi yatahojiwa. Lakini huu sio uamuzi wa kanza wa Mahakama hiyo kwa Tanzania. Uamuzi wa sasa utakuwa na tofauti gani? Fulgence Massawe ni wakali aliyebobea katika masuala ya haki za binadamu.
"Kuna mabadiliko kidogo ya kanuni za Mahakama, kama utasikia amri nyingi zilizotolewa, mwishoni wanaipa Tanzania muda wa kuleta taarifa ya utekelezaji wa maamuzi. Huko nyuma maamuzi yalikuwa yanatolewa lakini inaachiwa nchi yenyewe ikatekeleze maamuzi inavyotaka, lakini kwa sasa kuna mfumo unayoipa mahakama mamlaka ya kuita nchi ili itoe taarifa kwa namna gani wametekeleza kwahiyo ni suala ya muda.”
Mahakama hiyo ya haki za Binadamu inayo mamlaka kisheria ya kupinga maamuzi ya Mahakama za ndani na kutoa uamuzi wa juu unaozingatia viwango vya haki za binadamu barani Afrika.