1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mahakama ya Burundi yaamuru Ndayishimiye aapishwe

12 Juni 2020

Mahakama ya kikatiba nchini Burundi imeamuru kwamba rais mteule wa nchi hiyo, Evariste Ndayishimiye aapishwe baada ya kutokea kifo cha Rais Pierre Nkurunziza mwanzoni mwa wiki hii.

Evariste Ndayishimiye
Picha: Reuters/E. Ngendakumana

Ndayishimiye, alishinda uchaguzi wa rais mwezi Mei, na alitarajiwa kukabidhiwa madaraka mwezi Agosti, lakini sasa ataapishwa haraka iwezekanavyo. 

Mahakama hiyo ya juu ya Burundi imesema katika taarifa kwa waandishi wa habari kwamba hakuna haja ya kuwa na kiongozi wa mpito na kwamba rais mteule anapaswa kuapishwa haraka iwezekanavyo. 

Kifo cha Rais Nkurunziza siku ya Jumatatu akiwa na umri wa miaka 55, kimetokea siku kadhaa baada ya kuchaguliwa kwa mrithi wake Ndayishimiye, ambaye alitarajiwa kutawazwa mnamo mwezi Agosti.

Hali hiyo isiyo ya kawaida imezusha maswali juu ya namna kipindi cha mpito kingesimamiwa, wakati ambapo katiba inasema spika wa bunge la taifa ndiye anapaswa kuchukua uongozi pale rais wa taifa anapofariki. 

Majaji wa Mahakama ya Kikatiba ya BurundiPicha: Getty Images/AFP/T. Nitanga

Mkuu wa mahakama hiyo, Charles Ndagijimana akisoma uamuzi huo amesema wamezingatia katiba ya nchi na sheria nyingine muhimu zinazohusiana na utaratibu wa kukalia kiti cha urais. Mkuu wa mahakama ya kikatiba amesema wamepata kibali kinachothibitisha kufariki kwa Rais Pierre Nkurunziza. Hivyo wameamuru kuwa hakuna haja ya kuwepo na kipindi cha mpito, wakati yupo rais aliyeshinda uchaguzi ulofanyika mwezi uliopita.

''Tukizingatia kipengele nambari 121 cha katiba kwenye mstari wake wa pili, tunakuta nia na mwanasheria ya kuepusha pengo kwenye kiti cha rais katika muda huu baada ya kifo cha rais na kabla ya kutawazwa rais mteule. Pia mahakama ikizingatia kibali cha kuhakikisha kifo cha Rais Pierre Nkurunziza, inabaini kuwa hakuna kipindi cha mpito kinachoagizwa ili kuanda uchaguzi, kwa lengo la kupatikana rais mpya. Hivyo mahakama inaagiza Evariste Ndayishimiye aapishwe haraka iwezekavyo,'' alifafanua Ndagijimana.

Uamuzi huyo wa mahakama ya kikatiba umetolewa baada ya baraza la mawaziri wa serikali katika kikao chake kilichoongozwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Gaston Sindimwo kuitaka mahakama hiyo kubaini mwelekeo wa kisheria kuhusu nani atakayekalia kiti cha urais, baada ya kutokea kifo cha Rais Nkurunziza.
 

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW